Watanzania wote wameombwa kuwa tayari kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kwa mwaka 2012 sambamba na uandikishaji wa vitambulisho vya Uraia Tanzania linafanikiwa vyema kwa Maendeleo ya Taifa.
Ombi hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Piter Pinda wakati akizindua Kampeni ya uhamasishaji Sensa ya Watu na Makazi zilizofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Mjini Dar es salaam. Mh. Pinda alisema Taifa bila ya kuwa na Takwimu sahihi Serikali haitakuwa na uhakika wa kuwapangia Watanzania Mipango bora ya Maendeleo.
Alisema changamoto iliyopo hivi sasa kwa Viongozi wote ni kuhakikisha Jamii inaelewa umuhimu wa zoezi la Sensa kwa vile Takwimu zake zitatumika kwa lengo la kustawisha Jamii kupitia miradi ya Kiuchumi.
Mwenyekiti huo wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa amewasihi baadhi ya Viongozi wa Kidini kutochanganya dini na Sensa ambayo yanaweza kuvuruga lengo la Taifa la kuandaa zoezi hilo ambalo tayari limeshagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 141 hadi sasa. Hata hivyo Mh. Pinda amewapongeza Waumini wa Dini ya Kiislamu ambao tayari wameshaelewa umuhimu wa zoezi hilo la Sensa lisilohusiana kabisa na masuala ya Dini.
“ Watanzania ambao wako makini nina matumaini kwamba wataungana katika kufanikisha sensa wakati Taasisi na Mashirika ya Kimataifa yakisubiri matokeo ya Takwimu zitakazowapa mwanga wa namna ya kusaidia miradi ya Serikali na ile ya Kijamii Nchini”. Aliisitiza Mh. Pinda.
“ Usipofanya hivi na kukataa suala hili maana yake unakataa maendeleo wakati Serikali imeshatumia fedha nyingi”. Mwenye kiti huyo wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa alifafanua zaidi.
Kwa upande wake Mwenyekiti Mwenza wa Kamati hiyo ambaye pia ni makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema yapo matumaini makubwa ya mafanikio kutokana na juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na watendaji wote wanaohusika na matayarisho ya sensa.
Hata hivyo Balozi Seif alisema zipo changamoto za uelewa mdogo wa Wananchi juu ya umuhimu wa sensa kwa maendeleo ya Taifa uliochangiwa na baadhi ya Viongozi wa makundi ya dini kuwakataza wafuasi wao kutoshiriki katika zoezi hilo la sensa.
Alisema kitendo hicho kitawanyima wananchi hao haki zao za msingi za maendeleo ya kiuchumi na kijamii na hivyo inaweza kusababisha tofauti za kimaendeleo katika baadhi ya maeneo hapa nchini. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiwa pia ni Mwenyekiti mwenza wa Kamati hiyo aliwaasa viongozi hao wa kidini waelewe kwamba ushawishi wao huo utakuwa hasara kubwa kwa Taifa na kwa wananchi wote na kazi yao haitakuwa kwa faida ya mtu au kikundi chochote kile.
Ameziomba kamati mbali mbali za sense katika ngazi za Mikoa na Wilaya kuzitumia vyema siku chache zilizobakia katika kukamilisha maandalizi ya sensa na kuhamasisha wananchi kwenye maeneo yao kushiriki kikamilifu kaika zoezi la sense wakati utakapowadia.
Balozi Seif amewaomba pia wana habari waendelee na kazi ya kuhamasisha wananchi kupokea wito wa Serikali wa kila Mwananchi kuhesabiwa na hivyo kutimiza wajibu wake.
Akitoa salamu za Mashirika na Taasisi za Kimataifa yanayofanya kazi hapa Nchini Tanzania, Kaimu Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa Bibi Vibeke Johnson alisema utambuzi wa idadi ya Watu katika Taifa lolote lile unasaidia kuharakisha mipango ya Maendeleo.
Bibi Vibeke aliihakikishia Serikali ya Tanzania kwamba Mashirika na Taasisi za Umoja wa Mataifa zitaendelea kuunga mkono juhudi za Tanzania katika mipango yake ya Maendeleo likiwemo zoezi la sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.
Mapema Naibu Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Saada Salum alisema zoezi hili la Sensa ya Watu na Kakazi ni miongoni mwa mambo yaliyopewa kipaumbele na Serikali kwa mwaka huu wa 2012.
Mh. Saada amewakumbusha Wananchi wote Nchini kutunza kumbu kumbu zao zote za wana kaya ikiwemo ile muhimu ya waliolala katika kaya hizo usiku wa kuamkia tarehe 26 Agosti mwaka huu.
Alisisitiza kwamba Taarifa zote zitakazokusanywa wakati wa zoezi la sensa ni siri na zitahifadhiwa kwa mujibu wa sheria ya Nchi kupitia Takwimu nambari 351.
Uhamasishaji wa Sensa ya watu na makazi iliyozinduliwa utakaochukuwa takriban siku nane utaendelea hadi usiku wa kuamkia tarehe 25 kuingia tarehe 26 agosti siku ya zoezi lenyewe litakapoanza linalotajajiwa kuchukuwa siku saba.
Wakati huo huo Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 imekutana chini ya Mwenyekiti wake Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Pinda hapo katika Ofisi yake Mjini Dar es salaam.
Kikao hicho kiliendeshwa sambamba na Mwenyekiti mwenza wa Kamati hiyo ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kikihusisha pia Mawaziri na watendaji wa pande zote mbili za Muungano wa Tanzania.
Wakichangia baadhi ya mada zilizowasilishwa kwenye kikao hicho wajumbe wa kikao hicho wamesema juhudi bado zinahitajika kufanywa katika kuhamasisha wananchi kuelewa umuhimu wa Serikali wa kuleta zoezi la Sensa.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top