Chama cha Mapinduzi hivi sasa kinaendelea na utaratibu wa kuhakikisha Viongozi wanaoingia madarakani ndani ya chama kwenye chaguzi mbali mbali zinazoendelea unafikia Mahitaji yanayokidhi chama hicho kwa wakati huu wa sasa.
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akizungumza na Viongozi wapya, baadhi ya wanachama na Wananchi wa Jimbo hilo mara baada ya chakula cha mchana hapo katika Ofisi ya Jimbo la Kitope iliyopo Kinduni Wilaya ya Kaskazini B.
Utaratibu huo mpya aliouandaa Balozi Seif unakusudia kuunganisha ushirikiano na umoja miongoni mwa Viongozi wa Jimbo hilo ambao utakuwa wa kudumu muda wote wa utumishi wake ndani ya Jimbo hilo.
Balozi Seif aambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alisema Chama cha Mapinduzi kimekusudia kuongeza nguvu za kuendelea kuwa na Viongozi madhubuti ndani ya chama hasa wakati huu wa chaguzi zake.
Aliwatahadharisha wanachama wa chama hicho kuwa makini katika kipindi hichi kigumu cha mpito kuelekea kwenye mfumo wa katiba mpya ambacho tayari kimeibua baadhi ya Viongozi wa chama hicho kuwa na maneno yasiofanana na sera za CCM.
“ Lazima tuwe na Viongozi makini watakaoendeleza uwezo wa chama hicho kushinda kwenye chaguzi kuu zote zijazo hapa Nchini”. Alisisitiza Balozi Seif.
Aliwapongeza Viongoziwapya waliochaguliwa kushika nyadhifa mbali mbali za chama ndani ya jimbo hilo na waelewe kwamba wamechaguliwa kuondoza wenzao kwa kuzingatia maadili, bidii na uadilifu.
Balozi Seif alifahamisha kwamba imani ya wanachama kwa viongopzi hao itazingatia uongozi mzuri utakaokidhi mahitaji ya chama chenyewe na wanachama walioawachagua.
Amesema wakati umefika kwa wanachama wa CCM sehemu zote ni vyema wakawaepuka wanachama na viongozi viruka njia ambao wanaonekana kujichomoza ndani ya chama hivi sasa.
Akizungumzia siku kuu Balozi Seif aliwakumbusha Wazazi kuendelea kuwachunga Vijana wao katika kufuata maadili mema ambayo yamekuwa darasa zuri ndani ya kipindi kifupi kilichopita cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Alisema kufanya hivyo ndio njia pekee ya kudhihirisha kwamba yale mafunzo yaliyopatikana ndani ya mwezi huo yamepatikana na kukidhi lengo lililokusudiwa.
“ Tujitahidi sana kufanya ibada muda wote tulionao katika maisha yetu kwa kuendelea kufanya mazuri yanayotakiwa katika maamrisho ya muumba na vitanu alivyoteremsha”. Alikumbusha Balozi Seif.
Akimkaribisha Balozi Seif katika hafla hiyo Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mh. Pemba Juma Khamis alisema utaratibu huo aluouandaa balozi Seif unaonyesha jinsi gani anavyowajali wapiga kura wake katika masuala ya Jamii.
Mapema Mbunge wa Jimbo la Mpendae ambaye alipata mualiko wa kushiriki hafla hiyo Mh. Salum Turky aliwapongeza Wanachama wa CCM na Wananchi wa Jimbo la Kitope kwa uamuzi wao wa kumchagua Mbunge anaye jail kwa kuwaunganisha Wananchi katika harakati zao za Maendeleo na Kijamii.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top