Waumini wa Dini ya Kiislamu wamekumbushwa kuwa  tayari kuwarithisha  watoto wao mambo ambayo yanamridhisha  na kumfurahisha Mwenyezi Muungu likiwemo lile kubwa la kuhifadhisha Quran kwa lengo la kuwa na Viongozi makini wa dini hiyo hapo baadaye. 
Kumbusho hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akitoa nasaha zake kwenye  kilele cha mashindano ya kuhifadhi Quran yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo cha Kiislamu cha  Al-Haramain Mjini Dar es salaamu.   
Balozi Seif alisema ni vyema kwa Walimu wa vyuo vya Quran wakafikiria  kufundisha Kitabu hicho pamoja na Tafsiri yake hata kwa kiwango cha Juzuu 15 ili kuwajengea Vijana kupenda mambo yote mawili.   
Alisema kusoma na kuhifadhi Quran ni wajibu wa kila Muislamu ili ipatikane faida  ambayo imekusanya mahitaji ya viumbe vyote hapa Duniani.  
Alitahadharisha baadhi ya Waumini kujiepusha na tabia ya kutafsiri Quran kwa manufaa binafsi na kutoa wito kwa waumini hao kuendelea kushirikiana ili kuwa na nguvu katika mambo yao.     
 “ Ndani ya Kitabu hichi kuna mahitaji yetu yote ya kilimwengu na kesho akhera. Tutapataje mahitaji yetu yote bila ya kuifahamu Qurani?”.  Alihoji Balozi Seif.   
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Kamati ya maandalizi ya Mashindano hayo pamoja na wafadhili wote kwa juhudi za kufanikisha jambo hilo la kheri litakalowajengea hatma njema ya baadaye.   
Balozi Seif alisema hakuna kujuta katika kutoa kwa vile uwekezaji huu malipo yake huendelea dama bila ya kikomo. Akizungumzia suala la mwezi mtukufu wa ramadhani Balozi Seif aliwaasa waumini wenye tabia ya kusali mwezi mtukufu wa ramadhani pekee kuacha tabia hiyo inayokwenda kinyume na maamrisho ya Dini. 
 Alisema si vyema kwa waumini kuchagua mwezi wa kufanya ibada kwani muumini anawajibika kusimamisha sala kila siku katika kipindi chote cha siku 365 za mwaka mzima pamoja na kufanya mambo yote ya kheri. 
Mapema akisoma risala Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania { Bakwata } Ukti Shamim Khan alisema lengo la mashindano hayo ni kuwatia moyo Vijana kuipenda Quran ambayo itawasaidia kuongoka kwa kuelekea kwenye ucha mungu.   
Ukti Shamim alielezea masikitiko yake kuona walimu wanaowaandaa Vijana hao kwa muda mrefu sasa wanasahauliwa.  Alisema kazi yao ni nzito kinyume na kuangaliwa kama walimu wengine wa skuli za kawaida zinazotoa elimu ya Dunia.   Alifahamisha kwamba elimu ya Dini  ni vyema ikaenda sambamba  na elimu ya dunia  katika hatua za  walimu hao kujengewa  mazingira ya uwezeshaji. 
Akimkaribisha Mgeni Rasmi katika hafla hiyo Kaimu Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Ali Muhidini alisema Quran lazima ifanywe kuwa dira katika maisha ya kila siku ya waumini wote.  Sheikh Ali Muhidini alisema ukosefu wa vijana wengi kutoelekezwa katika elimu ya dini kumesababisha utitiri wa watoto wa mitaani unaosababishwa na ukosefu wa malezi bora.   
“ Mzazi kutompelekea mtoto wake kupata elimu ya Quran ni moja ya njia ya kuporomosha chini Quran”. Alisisitiza Kaimu Mufti Mkuu wa Tanzania.    
Sheikh Ali Muhidini alizionya baadhi ya kampuni za simu zinazoendesha utaratibu wa  maongezi ya kutaja pokea wimbo huu na matokeo yake quran kuacha mara moja utaratibu huo ambao unadhalilisha Kitabu cha mwenyezi muungu.  
Zawadi mbali mbali zmetolewa kwa washindi wa mashindano hayo ikiwa ni pamoja na Laptop Printer,tv, misahafu , fedha ambazo washindi wamefunguliwa akaunti Benki ya Amana.     
Mashindano hayo yamefadhiliwa na Benki ya Watu wa Zanzibar, Amana Benki pamoja na Rehema Foundatin inayofadhili wanafunzi katika vyuo mbali mbali ndani na nje ya nchi. 
Othman Khamis Ame 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa

0 comments:

 
Top