Usimamizi mbovu unaoendelea kufanywa na Baadhi ya Viongozi wa Serikali ikiwemo uzuwiyaji wa vikosi vya diria kufanya kazi zake ipasavyo umepelekea kuongezeka kwa uvuvi haramu katika ghuba ya Chwaka.
Kauli hiyo imetolewa na Wananchi wa Kijiji cha Marumbi walipokuwa wakielezea matatizo wanayopambana nayo mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipokutana nao kujua tatizo la kiini cha mgogoro usiopunguwa miaka 31 sasa ndani ya ghuba hiyo.
Bwana Ufuso Haji Haji akiwakilisha Wananchi hao katika mazungumzo hayo alisema sheria za uvuvi zipo lakini kinachosikitisha ni kuona baadhi ya Viongozi wa Serikali kuzifumbia macho na hatimae kuaachia baadhi ya wavuvi kuendeleza uvuvi haramu. Alisema wakati wanakijiji wanapigania kudhibiti uvuvi haramu wapo Viongozi wa Serikali wanaotumia nyadhifa na vyombo vyao vya uvuvi kuwapa wavuvi wengine wasiojali udhibiti wa hali hiyo.
“ Huu ni wakati mgumu sasa kwa vile tumefikia wakati tukiamini kwamba Serikali inajaribu kutuchezea wanakijiji wa marumbi na ndio maana tumefikia hatua ya kutokubaliana na lolote. Vyenginevyo labda aje Rais wa Nchi hapa”. Alisisitiza Bwana Ufuso.
Alisisitiza kwamba Wananchi wa Marumbi hawatakua tayari kwa lolote hadi tatizo lao la kuharibiwa Mashua zao zilizochomwa moto Tarehe 28/2/2012 litakapotatuliwa.
Akitoa nasaha zake kwa Wananchi hao wa Marumbi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amekiagiza Kikosi cha Kuzuia Magendo KMKM kuanzia sasa kufanya kazi zake za doria kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Balozi Seif amewaahidi Wananchi hao kwamba akiwa mtendaji Mkuu wa Serikali atahakikisha anasimamia kwa nguvu zote kukabiliana na tatizo la uvuvi haramu hapa Nchini.
“ Kuanzi sasa tutakwenda kutoa amri kwa KMKM ifanye wajibu wake wa kulinda uvuvi haramu unaofanywa na wavuvi wakorofi”. Alisisitiza Balozi Seif .
Alisema kama wapo Viongozi wanaoruhusu uvuvi haramu wajue kwamba wanafanya makosa makubwa . Balozi Seif katika Mkutano huo amekabidhi jumla ya Shilingi 6,000,000/- kwa ajili ya kusaidia wavuvi walioharibiwa nyavu zao na kuahidi atazungumza na Viongozi wenzake ili kulipatia ufumbuzi tatizo la mashua zao mbili zilizo haribiwa mapema mwaka huu.
Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipokea mchango wa maafa wa shilingi milioni kumi {10,000,000/- } kutoka kwa Uongozi wa Benki Kuu ya Tanzania { BOT }.
Mchango huo umewasilishwa na Mkurugenzi wa BOT Tawi la Zanzibar Nd. Joseph Mhando kwa niaba ya Gavana na Uongozi mzima wa Makao Makuu ya Benki hiyo yaliyopo Mjini Dar es salaam.
Akiwasilisha mchango huo Nd. Mhando alisema uongozi wa Benki hiyo umefarajika na hatua zilizochukuliwa na Serikali pamoja na Vikosi vya Ulinzi kwa usimamizi mzuri uliofanikisha zoezi zima la uokozi wa Watu waliokuwemo kwenye Meli iliyozama ya M.V. Skagit hivi karibuni.
“ Tunastahiki kuipongeza Serikali kupitia washirika wake hasa Vikosi vya Ulinzi na Uokozi kwa kuendesha zoezi zima la uokozi katika mazingira magumu kabisa”. Alisisitiza Ndugu Joseph.
Mkurugenzi huyo wa Benki Kuu ya Tanzania Tawi la Zanzibar amewaombea malazi mema wale waliotangulia mbele ya haki na kuwatakia maisha ya furaha wale waliookoka kwenya ajali hiyo mbaya.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali imesikitishwa na ajali hiyo kwa vile imezigusa familia za pande zote za Muungano.
“ Janga hili liliikumba Tanzania yote kwa sababu waliosafiri na chombo hicho walikuwa na asili ya pande zote za Tanzania”. Alifafanua Balozi Seif Ali Iddi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliuelezea ujumbwa Uongozi wa Benki hiyo ya Tanzania kwamba Baraza la Usalama la Taifa limeshaamua na kuagiza Meli zote zinazoagizwa au kununuliwa ni lazima zipate ridhaa ya kukubalika Kitaalamu kutoka kwa Mamlaka zinazosimamia usafiri wa Baharini.
Alisema hadi sasa maiti zilizopatikana kutokana na ajali hiyo ya Meli zimefikia watu 136, waliookolewa hai ni Watu 146, watu wanane bado hawajapatikana kwa mujibu wa idadi ya abiriwa 290 waliokuwa wameandikishwa kusafiri na Meli hiyo ya M.V.Skagit kutoka Bandari ya Dar es salaam kuelekea Zanzibar.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top