Mjumbe wa Kamati wa Siasa ya CCM Wilaya ya Kaskazini B Mama Asha Suleiman Iddi akiufungua Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Jimbo la Kitope. Mkutano huo umefanyika katika Ofisi ya CCM Jimbo la Kitope iliyopo Kinduni Wilaya ya Kaskazini B.
Tabia ya baadhi ya Wazazi waliowengi kuwa mbali na Watoto wao kwa kipindi kirefu imepelekea kupungua kwa malezi bora ya kundi kubwa la Watoto miongoni mwa Jamii hapa Nchini.
Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM ya Wilaya ya Kaskazini “B” Mama Asha Suleiman Iddi aliyaeleza hayo wakati akiufungua Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Jimbo la Kitope uliofanyika katika Ofisi ya CCM ya Jimbo hilo iliyopo Kinduni Wilaya ya Kaskazini B.
Mama Asha alisema hivi sasa ni nadra kukuta Wazazi wako pamoja na Watoto wao katika kuwaelekeza kwenye Mila na Silka sahihi zinazokubalika na Jamii.
Amewakumbusha Wazazi Nchini kuendelea kuwaasa watoto wao kujiepusha na majanga ya Dunia yaliyomo likiwemo kubwa zaidi la mabadiliko ya Maadili yaliyoukumba Ulimwengu kwa kisingizio cha Utandawazi.
“ Si rahisi hivi sasa kukuta wazazi wanaendeleza Malezi ya Pamoja katika Mitaa kama tulivyokulia sisi ambao bado tunaheshimu mila, Silka na Tamaduni zetu ipasavyo”. Alisisitiza Mama Asha.
Mjumbe huyo wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Kaskazini B aliwataka Viongozi kujenga tabia ya kusaidiana ili kukabiliana vyema na changa moto zinazoikabili Jamii
Alisema tabia ya kufikiria kila jambo linawahusu Viongozi wa ngazi ya juu kwa kulitafutia ufumbuzi linaweza kulipeleta Taifa mahali pabaya na hatimae kujenga dhana ya kuendelea kulaumiana kusiko na msingi.
Akizungumzia suala la Uchaguzi wa Jumuiya hiyo ya Wazazi Mama Asha aliwaomba Viongozi watakaoshinda na wale watakaoshindwa katika uchaguzi huo kuacha kuendeleza makundi mara tu baada ya kumalizika kwa zoezi hilo la uchaguzi.
Alisema hatua hiyo ielekezwe zaidi kwenye kushirikiana katika kukijengea uwezo wa kiutendaji Chama chao kwa lengo la kuandaa mazingira sahihi ya ushindi ifikapo mwaka 2015.
Akitoa Taarifa ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM Jimbo la Kitope Mjumbe wa Jumuiya hiyo Nd. Abdulla Luo alisema lengo la Jumuiya hiyo kwa kipindi kijacho ni kuendelea kuhamasisha Vijana kujua azma ya Chama ya kujenga Ustawi wa Jamii kupitia sera zake.
Nd. Luo alisema hatua hiyo imekuja kufutia baadhi ya Vijana kukumbwa na wimbi la kujiingiza katika vurugu za kisiasa kwa kisingizio cha dini.
Alisema kutokana na Vijana wengi kuachwa huru kwa kipindi mrefu kumepelekea hali ya kisiasa katika eneo hilo kutokuwa na utulivu wa kawaida.
Jimbo la Kitope lenye Matawi ishirini na CCM na Wadi nne limejipangia kuongeza Wanachama zaidi wa Jumuiya hiyo kutoka 958 waliopo hivi sasa.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top