Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano na Vikosi vya Ulinzi, pamoja na Taasisi za Kiaraia imepongezwa kwa hatua iliyochukuwa katika kukabiliana na Maafa yaliyotokea ya kuzama kwa Meli ya M.V. Skagit wiki iliyopita.
Pongezi hizo zimetolewa na Uongozi wa Taasisi tofauti zinazoendelea kutoa mkono wa pole hapa Zanzibar kufuatia vifo vya watu kadhaa waliokuwemo ndani ya Meli hiyo iliyopata ajali karibu na Kisiwa cha Chumbe.
Afisa Uhusiano wa Mfuko wa Pencheni { PPF } Bibi Lulu Mengele Bishop Michael wa Kanisa la Anglicana Dayosisi ya Zanzibar pamoja na Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu { UAE } Bwana Mallallah Mubarak Alameri wakitoa mkono huo wa pole kwa Balozi Seif walisema hatua hiyo imesaidia kuokoa maisha ya wananchi kadhaa.Walisema walio wengi wameshuhudia jitihada hizo za uokozi zilizoleta matumaini ndani ya nyoyo za Jamii.
Hata hivyo wawakilishi hao wa taaasisi tofauti walisema licha ya juhudi hizo za Serikali lakini bado ipo haja ya msingi ya kufuatwa kwa sheria na Taratibu sa usafiri wa Baharini.
Walisema utaratibu huo mbali ya kupunguza zinazoweza kuepukwa lakini pia utasaidia kuondosha mwanya kwa Wafanyabiashara na Wawekezaji wakorofi wanaoendesha biashara hiyo ya vyombo vya usafiri wa Baharini.
“ Kitu cha msingi ni kufuatwa kwa sheria na taratibu za usafiri nah ii itaondosha uzembe na ujanja unaotumiwa na wafanyabiashara wakorofi”. Alisisitiza Balozi wa UAE Bwana Mallallah.
Naye kwa upande wake Bishop Michael wa Kanisa la Anglikana la Mkunazini Dayosisi ya Zanzibar amesema hatua za serikali za kurejesha hali ya amani kufuatia fujo za baadhi ya Vijana zilizofanywa hivi karibuni imeleta faraja kwa waumini wa kanila lao.
Bishop Michael alisema Uongozi wa Kanisa hilo utaendelea kuwaelimisha Waumini wao kulinda na kuheshimu amani ya Taifa ambayo inahitajiwa na kila mwana Jamii.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Viongozi wa Serikali wanaendelea kupata matumaini kuona Taasisi na mshirika mbali mbali ndani na nje ya Nchi yanaunga mkono juhudi za Serikali.
Balozi Seif alisema Serikali kwa upande wake itaendelea kuchukuwa hatua madhubuti ili kuzuia majanga yanayoweza kuwepukwa ambayo yamo ndani ya uwezo wa mwanaadamu.
“ Tumeanza kuchukuwa hatua za kukabiliana na hali hii kwa kuwaomba washirika wetu ndani na nje ya Nchi kutusaidia katika sekta hii Likiwemo hili zito la upatikanaji wa meli kubwa ya usafirishaji wa wabiria na mizigo”. Alifafanua Balozi Seif.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top