Wananchi wameombwa kutoa Ushirikiano kwa Makarani wa Sensa kwa kutoa taarifa sahihi za kaya zao ili kupata takwimu sahihi kwa ajili ya Mipango ya Manedleo Nchini.
Ombi hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Al Iddi wakati akifunguwa Mafunzo ya siku 12 kwa Wakufunzi wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 ngazi ya Mkoa yanayoendelea huko chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu.
Balozi Seif ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Taifa ya Sensa Tanzania alisema ni vyema Wananchi wakatunza kumbu kumbu za Taarifa za maswali yatakayoulizwa kwa Watu wote watakaolala katika kaya zao usiku wa kuamkia siku ya Sensa.
Alisema kumbu kumbu hizo ndizo zitakazotumiwa kujibu maswali watakayoulizwa na Makarani wa Sensa siku watakayofika katika kaya zao katika kipindi cha kuhesabu Watu.
Hata hivyo Balozi Seif alisisitiza kwamba kazi ya kuhesabu kamwe haitasimamisha shughuli za Kiuchumi au Kijamii kwa vile Makarani wa Sensa watapita katika kaya zao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikumbusha kwamba kila Mtu atakayelala Nchini Usiku wa kuamkia siku ya Sensa ikimaanisha tarehe 25 kuamkia tarehe 26 Agosti Mwaka 2012 lazima ahesabiwen na hesabu hiyo ni mara moja tu.
Aliwataka Wakufuzi hao kuwa makini katika utekelezaji wa Majukumu yao hasa watakaporudi kutoa mafunzo Wilayani kwa lengo la kujenga mazingira bora ya kufanikisha zoezi hilo muhimu.
“ Tunahitaji Wakufunzi kuwa makini. Mkiburunga hapa maana yake mtakwenda kuburunga huko muendako kutoa Taaluma”. Alitahadharisha Balozi Seif.
Alipendekeza ile sifa ya Tanzania ya kufanya vyema katika Sensa ya Mwaka 2001 na kupata Heshima kubwa katika nyanja ya Kimataifa inapaswa kulinda na kuenziwa.
Alisema mbali ya mafanikio hayo kuwa darasa kwa Mataifa Kadhaa Barani Afrika lakini pia Tanzania ilichaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa  kwa kipindi cha miaka mine kuanzia mwaka 2012.
Balozi Seif alielezea matumaini yake kwamba uzoefu, Taaluma na umakini walionao Wakufunzi hao watazingatia mafunzo yao ili kuhakikisha kwamba wanaifanya kwa weledi na ufanisi mkubwa zaidi kuliko ule wa mwaka 2001.
Akizungumza na Vyombo mbali mbali vya Habari mara baada ya hotuba yake kuhusiana na Ushiriki wa Waislamu katika suala la Sensa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali itajitahidi kuzungumza na Viongozi wa Taasisi za Kidini ili kuondoa ushawishi unaoweza kuvuruga zoezi hilo.
Balozi Seif aliongeza kusema kwamba kutokana na umuhimu wa Takwimu za Sensa kwa ustawi wa Jamii ni vyema Taasisi za Kidini zikashirikiana na Serikali katika ufanisi wa suala hili muhimu kwa Umma linafanikiwa vyema.
Mapema Kaimu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Ali Juma Shamhuna alisema Takwimu za Sensa kwa kiasi kikubwa  zitaliwezesha Taifa  kupanga Mipango sahihi ya Maendeleo.
Waziri Shamuhuna alisema Serikali imejiandaa kufanya Sensa ya Watu tarehe 26 Agosti ili kujua Rasilmali Watu Nchini kwa kupitia utaratibu huu wa Sensa.
Alisema mbali ya mambo hayo lakini pia Takwimu hizi kwa mwaka huu zitaweza kusaidia kutathmini Mpango wa Taifa wa kupunguza Umaskini Zanzibar { Mkuza } na ule wa Bara Mkukuta sambamba na dira 2020  kwa Zanzibar na 2025 kwa Tanzania Bara.
Mafunzo hayo ya Wakufunzi wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ngazi ya Mkoa yataendelea hadi Tarehe 27 Mwezi huu wa Julai Mwaka 2012.
Othman Kahmis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top