Kikao cha Kamati ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi Tanzania kimefanyika Mjini Zanzibar Chini ya Mwenyekiti wake Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Pinda.
Sambamba na Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Hiyo Balozi Seif Ali Iddi kikao hicho kilichoshirikisha pia Wajumbe wa pande hizo mbili za Muungano wakiwemo watendaji wa Kamati hiyo kilifanyika kwenye ukumbi wa jumba la Wananchi Forodhani Mjini Znzibar.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Albina Chuwa alisema pamoja na mambo mbali mbali Uongozi wa Kamati ya Sensa umeshafanya mazungumzo kati yao na Viongozi wa Dini mbali mbali Nchini na kuleta matumaini.
Mtakwimu Mkuu huyo wa Serikali alimpongeza Mufti Mkuu wa Tanzania kwa kutoa Tamko la kuwataka Waumini wa Dini ya Kiislamu Nchini kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu wakati utakapowadia.
Dr. Albina alifahamisha kwamba Serikali Kuu tayari imeshatuma jumla ya Shilingi Bilioni 1.7 kati ya hizo shilingi Milioni 215,000,000/- ni kwa Zanzibar kwa ajili ya kuendeleza Elimu ya Sensa Mikoani.
Akizungumzia suala la maandalizi ya uhamasishaji umma Dr. Albina alifahamisha kwamba utekelezaji wa kutumia vyombo vya Habari hasa vile vya Jamii tayari umeanza kwa Wahariri, Waandishi na Wakuu wa vyombo hivyo kwa kupatiwa mafunzo yatakayowasaidia kutoa elimu kwa Jamii juu ya ufahamu wa zoezi hilo muhimu kwa Taifa.
Wajumbe kadhaa ywa Kikao hicho katika kutoa mawazo yao walielezea umuhimu wa Mabaraza ya Madiwani kupewa mamlaka na jukumu la kutoa Elimu katika Halmashauri zao.
Kikao cha Nne cha Kamati hiyo ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi Tanzania kinatarajiwa kufanyika mkoa wa Pwani mnamo Tarehe  4 Agosti mwaka 2012.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top