Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Marekani kupitia Kampuni ya Light Years IP inaandaa Mpango wa Kibiashara utakaoiwezesha Zanzibar kuuza bidhaa zake kwa utaratibu utakaopunguza ushiriki wa wafanyabiashara wa kati na mawakala.
Mpango huo utatumia Tasnia ya mabunifu kwa bidhaa za Zanzibar na kufanya utambulisho maalum wa zao Kuu la Uchumi wa Taifa la Karafuu na baadae mazao mengine ya viungo yanayozalishwa hapa Zanzibar.
Hayo yamefahamika kufuatia mazungumzo ya pamoja kati ya  Timu ya Wizara ya Biashara iliyoongozwa na Waziri wake Mh. Nassor Ahmed Mazrui, Mwakilishi wa Kampuni ya Light Years IP Profesa Rom  Layton kutoka Marekani na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Profesa Rom alimueleza Balozi Seif kwamba hatua kadhaa tayari zimeshachukuliwa  kati ya pande hizo mbili katika harakati za  maandalizi za mpango huo.
Mtaalamu huyo wa Kampuni ya Light Years IP Profesa Rom alizitaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa kuwa ni pamoja na warsha ya uwelewa iliyoshirikisha watendaji wa Taasisi za Serikali pamoja na kuundwa kwa timu za wataalamu wa bidhaa za viungo.
Aidha alisema katika kufanikisha matayarisho ya mpango huo kampuni ya Light Years IP imeongeza mabingwa waliobobea katika fani hii ili kuisaidia Zanzibar kwenye matayarisho hayo  kwa lengo la kupenya katika masoko  ya Kimataifa kwa biadhaa zake za viungo ikiwemo Karafuu.
Mapema Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar Mh. Nassor Ahmed Mazrui alisema lengo la Serikali ni kuwanyanyua Wakulima  katika uzalishaji wenye tija.
Mh. Mazrui alisema mazao ya Viungo ikiwemo Karafuu yana tija kwa uchumi wa Zanzibar kutokana na ubora wa mazao hayo lakini uuzwaji wake uko katika kiwango cha chini katika masoko ya kimataifa hali inayopelekea kupungua kwa kipato cha Wakulima.
Alisema zaidi ya asilimia 95% ya mapato ya mazao ya viungo na Karafuu yanakwenda kwa wafanyabiashara wa kati na mawakala wakati asilimia 3% hadi 5% inakwenda kwa serikali hali inayotokana na udhaifu katika kuwafikia watumiaji wa mwisho kwenye soko.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika kuunga mkono Mpango huo muhimu kwa Taifa alisema Zanzibar bado inahitaji kuimarisha Mazao yake ya Viungo.
Balozi Seif alisema Mpango huo ni muhimu na mzuri kwa Wananchi na hasa Wakulima wa kawaida lakini tatizo kuu linalowaathiri ni mbinu na ubora wa kuyaweka vizuri mazao yenyewe ili kukithi hadhi ya soko la Kimataifa.
“ Tumekuwa tukishuhudia mara nyingi utaalamu wa kuhifadhi bidhaa unakuwa kikwazo na tatizo sugu kwa wananchi na wakulima wetu”. Alifafanua Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Balozi Seif alisisitiza kwamba wimbi hili pia limeikumba bidhaa ya Karafuu iyayozalishwa Zanzibar na hatimaye kutumiwa na Wafanyabiashara wa Nchi Jirani ambalo lilikuwa likiuzwa kimagendo katika soko la Kimataifa bila ya kuzingatia usafi halisi wa Zao hilo.
“ Wafanyabiashara hao walikuwa wakinunua Karafuu kimagendo, kuzichanganya pamoja daraja mbali mbali na hatimae kuziuza bila ya kuzingatia ule utaratibu halizi wa uhifadhi wa Kitaalamu”. Alikumbusha Balozi Seif.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top