Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepongezwa kwa uamuzi wake wa kuandaa mpango mpya wa nadharia ya Utalii kwa wote ambao umelenga kuwa na Wataalamu zaidi watakaosaidia Eneo la Utalii linayotarajiwa kuwa Sekta Kiongozi ya Uchumi wa Zanzibar.
Pongezi hizo zimetolewa na Ujumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Jumuiya ya Makampuni ya Watembeza Watalii Zanzibar { ZATO } ulipofanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Ujumbe huo ukiongozwa na Mwenyekiti wake Khalifa Makame ulimueleza Balozi Seif kwamba hatua hiyo ya Serikali imeleta faraja kwa washirika wengi wa Sekta hiyo ikiwemo Jumuiya yao.
Wamesema Jumuiya yao imeamua kuweka mikakati zaidi katika kuunga mkono mpango huo wa Serikali kwa kushirikisha zaidi Wananchi moja kwa moja katika masuala ambayo ni kivutio kwa wageni ambayo yamo ndani ya maeneo yao.
“ Kuna vyakula vya asili kama muhogo, ugari, majimbi na hata matunda yenye kuzalisha hapa Zanzibar yanaweza kuandaliwa utaratibu mzuri wa kuuzwa katika maeneo ambayo watalaii na wageni hutembelea”. Walisema wajumbe wa jumuiya hiyo.
Wajumbe wa Bodi hiyo ya Wakurugenzi wa Jumuiya ya Makampuni ya Watembeza Watalii Zanzibar { ZATO } walisisitiza kwamba mipango hiyo ni moja ya utaratibu unaoweza kumnufaisha moja kwa moja Mwananchi kujiongezea kipato”.
Walisema katika kwenda samba mba na sera ya Serikali Kuu ya Utalii kwa Wote Jumuiya yao inafikiria kufanya shughuli zao za kila siku kwa kutumia kadi katika malipo ili kudhibiti ubadhirifu kwa lengo la kuiongezea mapato zaidi Serikali.
Waliongeza kwamba taratibu zinachukuliwa na Jumuiya yao ya kutegemea kuanzisha Tamasha la Biashara hapa Zanzibar litakalotoa fursa kwa washirika wote wa sekta ya Utalii kutangaza Vitu na bidhaa zao wanazozalisha.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliueleza Ujumbe huo kwamba Zanzibar bado haijafanya Utafiti wa kina wa kujua Watalii na wageni nini wanakipenda au kukihitaji zaidi wakati wanapoingia Nchini.
Balozi Seif alisema tatizo linaloonekana ambalo ni la muda mrefu ni namna ya kujipanga zaidi na kuandaliwa mazingira mapya ambayo Mtalii anaweza kuvutika nayo.
Alizishauri Taasisi zinazosimamia Sekta ya Utalii kujipanga vizuri katika kuutumia muda wenye upungufu wa uingiaji wa wageni { low Season } uendelee kuwa wa kawaida kwa kuweka vishawishi vitakavyomfanya Mtalii aendelee kuja Nchini muda wote.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikutana na Ujumbe wa Kampuni inayozalisha Umeme kwa kutumia taka taka ya nchini Ufaransa { CITELUM } yenye Tawi lake Barani Afrika.
Mkurugenzi mkuu wa Kampuni hiyo kanda ya Afrika Bwana Pierre Doutreloux alimueleza Balozi Seif kwamba mradi wao umelenga zaidi kutoa huduma kwenye Miji mbali mbali samba na usafi wa Mji kutokana na maumbile ya mradi wenyewe.
Bwana Pierre alisema mradi huo hufanikiwa vyema katika maeneo husika baada ya jamii inayouzunguuka kupewa Taaluma ya kina ya namna ya matumizi ya ukusanyaji wa taka taka. Mradi kama huo unaotumia eneo la ukubwa wa Hekta 7 tayari umeanzishwa katika Miji ya Mexico, Brazil na Bukinafaso.
Balozi wa Heshima wa Jamuhuri ya Seychelles Nchini Tanzania Bibi Marry Vonne Pool aliyeuongoza Ujumbe huo alisisitiza kwamba upo umuhimu wa kusafisha Miji katika maeneo mbali duniani kwa kutumia mradi wa umeme unaotumia Taka taka.
Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ameelezea kuridhika kwake na Mipango ya Kampuni ya Citelum ya kuendeleza Mradi huo ambao ni ukombozi wa utunzaji wa Mazingira katika maeneo ya Mjini.
Balozi Seif aliuomba Ujumbe wa Uongozi wa Kampni hiyo kuendelea kukutana na Watendaji wa Taasisi mbali mbali Nchini ili kuangalia mazingira iwapo mradi kama huo unaweza kuwekezwa hapa Nchini.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top