Waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na Wazazi wanahitajika kuendelea kujenga Misingi ya Maadili imara ambayo inaonekana kulega lega hasa kwa Vijana kunakosababishwa na Mambo tofauti likiwemo la kukua kwa Mawasiliano ya Sayansi na Teknolojia Duniani.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akiiungua Ijitimai ya 17 ya Kimataifa inayofanyika katika majengo ya Jumuiya ya Fiy Sabilillah Tablih Markaz Fuoni Migombani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema Watanzania wengi hasa Vijana wamekuwa wakijijengea Utamaduni wa kuiga maadili mabovu badala ya kufanya mema ambayo yanakwenda kinyume na Mila, Silka na hata Taratibu za Dini.
Balozi Seif alitoa rai kuwa pamoja na mada nyengine zilizoandaliwa katika Ijitimai hiyo ni vyema kwa wahadhiri watakaopata fursa waitumie hadhara hiyo kujadili kwa kina mbinu zitakazosaidia kurejesha maadili mema miongoni mwa Vijana Nchini.Makamu waPili wa Rais wa Zanzibar alitahadharisha kwamba mmong’onyoko wa maadili ni tishio kwa Ustawi wa Taifa lolote lile hapa Duniani.
“ Siku hizi si jambo la ajabu kukutana na kundi la Vijana wa Kiislamu wanatumia dawa za kulevya zinazopelekea kujiingiza katika vitendo viovu”. Alitanabahisha Balozi Seif .
Akikumbusha suala la umuhimu wa Waislamu kufanya kazi, Balozi Seif alisema hakuta kuwa na njia ya mkato wa kuendesha afamilia bila ya kufanya kazi kwa bidii.Alisema Uislamu kupitia Kitabu kitukufu Qurani sdambamba na Hadithi zake imesisitiza umuhimu wa kufanya kazi za halali ili kuwa na sababu ya kujipatia chumo la halali.
Balozi Seif alikariri moja ya Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Mtume Muhammad { SAW } ikisema chumo bora ni lile mja alichumalo kwa mikono yake.
“ Tabia iliyojengeka katika Jamii yetu ya ubadhirifu wa Mali za Umma tukumbushane kuwa tabia hiyo haifai na tuachane nayo mara moja”. Alitahadharisha Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia waumini wa dini zote Nchini kwamba Serikali itaendelea kuheshimu uhuru wa kuabudu kwa kushirikiana na Taasisi zote za Kidini Nchini kwa lengo la kustawisha Jamii yote.
Alisema Katiba ya Nchi ijnaeleza wazi kwamba kila mtu ana haki ya kuabudu dini aitakayo mradi havunji sheria za Nchi.Kuhusu suala la Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba Viongozi wa Dini zote kuhamasisha wafuasi wao kushiriki kikamilifu katika zoezi la kuhesabiwa linalotarajiwa kufanyia usiku wa kuamkia tarehe 26 Agisti Mwaka huu.
Alisema Sensa ina manufaa mengi kwa maendeleo ya Taifa kwa vile takwimu itakayopatikana itatoa fursa kwa Serikali kuweza kujipangia Mipango ya Maendeleo kwa mujibu wa idadi ya watu waliopo.
Mapema Mwenyekiti wa Jumuiya ya Fiy Sabilillah Tablih Markazi Zanzibar Sheikh Ali Khamis aliiomba Serikali kuifanyia marekebisho sheria na kuweka adhabu kali kwa mtu anayekutwa au kutumia Dawa za kulevya.
Sheikh Ali Khamis alisema hali ya maasi iliyoshamiri Mitaani inatishia maisha ya Wananchi na Waumini kunakopelekea kukosa utulivu wa kufanya ibada na mambo yao ya kidunia.
“ Wizi wa kutumia nguvu,Ujambazi unaopelekea mauaji, ubakaji ambayo yote husababishwa na utumiaji unga ni mambo yanayoleta aiba nakusikitisha”. AlisisitizaSheikh Ali Khamis.
Zaidi ya Waumini Kiislamu wapatao 12,000 kutoka Nchi jirani za Afrika Mashariki, Mikoa 13 ya Tanzania Bara, London pamoja na Wenyeji Pemba na Umguja wamehudhuria Ijitimai hiyo ya 17 ya Kimataifa.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Mkamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

0 comments:

 
Top