Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameelezea umuhimu wa kuondoshwa sintafahamu iliyopo baina ya Wananchi wa eneo la Kisaka saka na Kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania {JWTZ } iliyopo katika eneo hilo ili kuendeleza ujirani mwema kati ya pande hizo mbili.
Balozi Seif alieleza hayo wakati akizungumza na Wananchi wa Eneo la Maungani, Kombeni na Fuoni pamoja na Uongozi wa Jeshi hilo baada ya kupokea malalamiko ya wananchi hao pamoja na Taarifa ya Jeshi hilo kufuatia tatizo la mipaka ya Ardhi lililojichomoza baina ya pande hizo mbili.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema hakuna haja ya uhasama kati ya Askari na Raia na kusisitiza kwamba pande hizo mbili ni vyema zikaendelea kuheshimiana. Balozi Seif aliagiza kuundwa mara moja kwa Kamati ya Pamoja Kati ya Uongozi wa Jeshi hilo na Wananchi hao kwa kushirikisha pia na Watendaji wa Taasisi zinazosimamia Suala la Ardhi chini ya Mkuu wa Wilaya ya Magharibi.
“ Hii Kamati naipa muda wa mwezi mmoja na Mkuu wa Wilaya ahakikishe ananiletea jibu la hatma muwafaka la tatizo hili ifipako mwishoni mwa Mwezi wa Agosti” Alisisitiza Balozi Seif.
Alifahamisha kwamba hakuna sababu ya kuendeleza mtafaruku baina ya Jamii na Taasisi za Serikali na kushauri hekima itumike zaidi wakati yanapojitokeza matatizo hasa ya ardhi. Balozi Seif alisema Taratibu za Askari kutumia ubabe wakati Wananchi watapandisha jazba katika kutafuta haki ya umiliki wa Ardhi kunaweza kuleta athari ya kudumu hapo baadaye.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliendelea kuikumbusha Jamii kwamba Ardhi itaendelea kuwa Mali ya Serikali jambo ambalo linaelezwa kila wakati.
Balozi Seif alifafanua kwamba Serikali wakati wote huamua kulipa fidia ya Majengo au Vipando kwa Wananchi watakaoathirika kutokana na Maamuzi yake ya kuitumia Ardhi hiyo kwa shughuli za Taasisi zake zinazohudumia Wana Jamii wote.
Alisema katika kukabiliana na tatizo la Ardhi Serikali imekuwa ikiendelea kutoa mafunzo kwa watendaji wake,Viongozi na hata Masheha ili kulielewa vyema suala hili linaloonekana kuleta migogoro kila kukicha.
“ Mimi na wasi wasi na suala hili la migogoro ya Ardhi kwamba baadhi ya Viongozi walio wengi wanaliogopa kwa kuhofidha lawama miongoni mwa wanaowaongoza kwa sababu semina tunatoa lakini utekelezaji wake ni hafifu”. Alifafanua Balozi Seif.
Mapema wakitoa malalamiko yao baadhi ya Wananchi hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya walalamikaji wa eneo hilo la Ardhi walielezea masikitiko yao kutokana na Jeshi hilo kutanua eneo la Mipaka ya Ardhi bila ya kushirikishwa wao katika awamu ya Pili sasa.
Wananchi hao waliomba kuwepo na mipaka ya kudumu ya eneo la Jeshi hilo itayokubalika na pande zote mbili kwa lengo la kuepuka migogoro inayoweza kudhibitiwa mapema. Akitoa Taarifa ya Kikosi cha 672 Mkuu wa Kambi hiyo iliyopo Kisaka saka Canal Omar Suleiman Mateka alisema kwamba ramani ya sehemu hiyo inaonyesha kuwa eneo hilo lilikuwa la malisho ya Mifugo wakati kambi hiyo inaanzishwa rasmi Mwaka 1978.
Canal Omar alieleza kuwa matatizo ya ardhi baina ya Jeshi na Wananchi walioizunguuka Kambi hiyo yamejichomoza Mwaka 2008 na kupelekea Mkuu wa Brigedia Nyuki kuagiza kufanywa kwa Vikao kwa pande husika katika miaka ya 20011 kufuatia Barua za Malalamiko kutoka Kwa Wananchi hao. Mkutano huo ulihusisha pia Naibu waziri wa Ardhi,Maendeleo ya Makaazi, Nishati na Madini Zanzibar, Watendaji wake pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Magharibi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top