Matatizo ya kutafuta Wafanyakazi wa Hoteli za Kitalii kutoka Nje ya Zanzibar yatapungua kwa kiasi kikubwa kama sio kuondoka kabisa iwapo Wanataaluma wa Chuo cha Mendeleo ya Utalii Zanzibar watatumia uwezo walionao katika kuwaandaa vyema wanafunzi wa fani ya Utalii.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la Jengo Jipya la Makataba ya Chuo cha Maendeleo ya Utalii liliopo Maruhubi Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema kilio kikubwa kiliopo cha Jamii na hasa Vijana cha waajiriwa wengi katika sekta ya Utalii kutoka nje ya Zanzibar ndicho kilichopelekea Chuo hicho kuwa na umuhimu wa pekee katika kukabiliana na tatizo hili.
Aidha Balozi Seif alieleza kwamba uimarishwaji wa Chuo hicho unalenga kukabiliana na visingizio vinavyotolewa na Wawekezaji wengi wa Hoteli na Taasisi zinazolingana ingawa utafiti umeonyesha visingizio hivyo sio vya kweli. Balozi Seif alisema Chuo cha Utalii kinaweza kufanya vizuri na kuleta Maajabu zaidi kulingananisha na mazingira halisi ya kuimarika na kukua kwa kasi Sekta ya Utalii hapa Nchini.
Alisisitiza kwamba lazima chuo kiendelee kubadilika kwa kasi kubwa sambamba na kasi ya ukuaji wa Sekta hiyo ya Utalii katika uimarishaji na Uendelezaji wa Uchumi wa Nchi na Jamii.
“ Kwa kuwa tunalalamikiwa kuhusu viwango vya Elimu vya Vijana wetu, Lazima Chuo kitoe Elimu inayolingana na mahitaji ya soko”. Alifafanua Balozi Seif.
Balozi Seif aliwaomba wanafunzi waliopo na watakaopita chuoni hapo kuwa majasiri, Mahiri na wabunifu katika kujiendeleza kielimu kwa lengo la kushika soko liliopo ili kuhudumia vyema sekta ya Utalii.
“ Nitafarajika sana sana iwapo matunda ya Taaluma inayotolewa na chuo hichi itakidhi malengo yaliyokusudiwa ya Wahitimu wake kuchukuwa nafasi kubwa katika soko la Ajira ndani na Nje ya Zanzibar”. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali imetilia mkazo upanuzi wa Chuo hicho ili kuondoa mazingira yanayokwaza utoaji wa mafunzo katika kiwango kinachotakiwa yakiwemo wanafunzi kusoma chini ya Mti na kukusanya wanafunzi wengi katika darasa moja.
Alisema ni vyema juhudi hizo za Serikali zikaenda sambamba na haja ya kuwa na Walimu wenye sifa zitakazokuza viwango vya ufahamu wa Wanafunzi.
“ Nataka Chuo hichi kiwe pekee na cha mfano katika kanda ya Afrika Mashariki. Hilo jengo la ghorofa moja lililokusudiwa kujengwa itapendeza kama litakuwa akali ghorofa Tano”. Alishauri Balozi Seif.
Balozi Seif aliagiza Wizara na Taasisi husika kufanya utafiti wa kuziangalia upya Sheria za kazi katika Seka ya Utalii ili zijenge mazingira bora ya upendeleo maalum kwa waajiriwa wa Hoteli kuwa wananchi wanaozizunguuka Hoteli husika.
Akitoa Taarifa fupi ya Chuo na Ujenzi wa Jengo hilo la Maktaba Mkurugenzi wa Chuo cha Maendeleo ya Utalii Zanzibar Bibi Zuleikha Kombo ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uamuzi wake wa kutoa ruzuku ya Ujenzi wa Jengo hilo muhimu.
Bibi Zuleikha alisema ujenzi huo utakwenda sambamba na ongezeko la idadi ya Wanafunzi kila mwaka hasa Vijana ambao tayari wameshapata muamko kutokana na umuhimu wa Sekta ya Utalii kwa Maendeleo ya Uchumi wa Taifa.
Akimkaribisha Balozi Seif Waziri wa Habari, Utamaduni,Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk alisema Serikali imeshaamua kuufanya Utalii kuwa Sekta Kiongozi ya Uchumi wa Zanzibar na tayari wizara yake imeshajenga matumaini makubwa na kuridhika na utendaji wa Chuo hicho.
Mh. Mbarouk alieleza katika kwenda sambamba na hatua hiyo chuo hicho kina Mpango wa Baadae wa kujenga Jengo la Kisasa la Wanafunzi na kufikia kiwango cha kutoa Shahada ya kwanza ya Fani ya Utalii kwa gharama ya shilingi Bilioni Nne { 4,000,000,000/- }.
Chuo cha Mendeleo ya Utalii Zanzibar kiliopo Maruhubi ambacho hivi sasa kina Wanafunzi 323 kinatoa Taaluma katika Fani ya Utalii, Kompyuta na Habari.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top