Jamii Nchini imeangizwa kujijengea utaratibu wa kufanya mazoezi ya Viungo kila siku ili kuimarisha miili yao sambamba na kujihakikishia uzima wa afya zao.Agizo hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mapema asubuhi wakati akikizindua Rasmi Kikundi cha Mazoezi ya Viungo cha Lulumba { Lumumba Fitness Club } hapo katika Uwanja wa Lumumba Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema Watu wengi hivi sasa wanaendelea kukosa mazoezi kutokana na kujidekeza kupenda usafiri hata kama utakuwa wa Kilomita moja tu. Alifahamisha kwamba Mazoezi wakati wote yanapunguza mambo mengi yasiyoleta faida kwa Jamii ambayo huonekana zaidi yakiwakumba Vijana walio wengi Mitaani.
“ Tuna mifano mingi na hai kwa Wazee wetu waliopita ambao walikuwa wakitembea masafa marefu yaliyowapa ukakamavu uliopelekea kuwajengea uzima zaidi wa Afya”. Alieleze Balozi Seif.
Aliagiza uimarishwaji wa Vifaa vya Mazoezi kwenda sambamba na Maadili na Utamaduni wa Taifa kwa lengo la kujenga mazingira bora ya Michezo hapa Nchini. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza suala la kuendelezwa kwa Amani miongoni mwa Wananchi ambayo ikitoweka hata muda wa kufanya mazoezi utakosekana.
Alisema suala la Amani ni la msingi muda wote katika harakati za Maisha ya kila siku na ni vyema likaimarishwa ndani ya Vilabu vya mazoezi. Akizungumzia suala la kuvipatia uwezo wa kujiendesha Kimaisha Vikundi hivyo vya mazoezi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali Kuu itaandaa utaratibu wa kutoa mkopo wa Vifaa
Kwa ajili ya kusukuma mbele miradi ya wana vikundi hao. Balozi Seif aameahidi kwamba changa moto zinazovikabili vikundi hivyo ambavyo vimeshapata usajili wa kudumu vinashughulikiwa kwa kupatiwa nguvu baada ya kubuni miradi ya kiuchumi.
“ Waziri anayesimamia Michezo Said Mbarouk amenisaidia katika maelezo yake hivyo tutashirikiana na Wizara yake katika kuona suala hilo linapatiwa ufumbuzi unaostahiki.
Katika risala yao Wanamichezo hao wa mazoezi wa Lumumba Fitness Club iliyosomwa na Naibu Katibu wa Kikundi hicho Hassan Mussa Mohd amesema kikundi chao mbali ya zoezi pia kimejiwekea malengo ya kushiriki katika kazi mbali mbali za Kijamii.
Hassan Mussa alisema tayari kikundi hicho kimejikita zaidi katika suala la utunzaji wa mazingira kwa kupata miti katika siku watazojipangia hapo baadaye kama Ujumbe wao unavyosema Mchezo na Maendeleo.
Wanakikundi hao wa Lumumba Fitness Club wamezitaja baadhi ya changa moto zinazowakabili kuwa ni pamoja na ukosefu wa Ofisi na Vifaa vya mazoezi pamoja na Fedha kwa ajili ya kuimarisha miradi ya Maendeleo waliyojipangia.
Akimkaribisha Mgeni rasmi Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk alisisitiza kwamba utaratibu wa kufanya mazoezi uwe wa kawaida na wa lazima kutokana na mabadiliko ya maisha yalivyo hivi sasa. Waziri mbarouk alikumbusha suala la kuendelezwa Mila na Silka katika kushajiisha mazoezi zitakazoambatana sambamba na Utumiaji wa Utamaduni.
“ Nitafurahi kuona Utamaduni wetu unatumika zaidi na vyema katika kuimarisha mazoezi kupitia michezo yetu”. Alifafanua Waziri Mbarouk.
Vikundi vilivyoshiriki sherehe hizo za uzinduzi wa kikundi cha Mazoezi cha Lumumba Fitness Club ni pamoja na Wonderers, Hatunshindwi, Namles. Kizazi kipya, Amani, Maisara, Obama, Chumbuzi Studios, Kitambi Noma, Muungano, Tupendane, Mandela,Nidhamu, Wasafi, Kata Presha Mwenge, Kizimkazi, Zaffias na wenyeji Lumumba Fitness Club.
Zaidi ya Shilingi 3,000,000/- zimeahidiwa kutolewa na Viongozi na Watu mbali mbali kusaidia kuchangia mfuko wa Kikundi hicho kufuatia mchango wa papo kwa papo ulioanywa kiwanjani hapo ambao pia uliambatana na utolewaji wa vyeti kwa washindi wa michezo mbali mbali.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment