Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa Msumbiji imekumbushwa
tena kufikiria ombi la Zanzibar
la kuipatiwa Wataalamu katika kuendeleza Sekta ya ufugaji wa Samaki wa Kamba.
Ombi hilo limetolewa na
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi wakati wa mazungumzo yake na Balozi wa Msumbiji Nchini Tanzania Bwana Zakaria Kupela yaliyofanyika hapo Ofisini
kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Msumbiji imekuwa
na uzoefu wa muda mrefu katika shughuli za ufugaji wa kamba na kujipatia umaarufu sehemu mbali mbali
Duniani.
Alisema utaalamu na uzoefu ulioipata Nchi hiyo unaweza
kuisadia Zanzibar
katika moja ya harakati zake za kujenga mazingira ya ajira kwa Vijana wake.
“ Sio mbaya kukukumbusha tena lile wazo letu
nililokuelezea wakati ule tulipokutana
kwa mara ya kwanza ingawa inaonekana kulikuwepo na tatizo la ufuatiliaji wa
suala hilo”.
Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
alimpongeza Balozi Mdogo wa Msumbiji Bw. Zakaria Kupela kwa juhudi zake za
kuendelea kuunganisha uhusiano uliopo kati ya Msumbiji na Tanzania na Zanzibar
kwa Ujumla.
Balozi Seif alifahamisha kwamba uhusiano wa pande hizo
mbili ni wa maumbile kutokana na maingiliano ya kidamu yaliyopo kati ya
Wananchi wa Tanzania
na Msumbiji.
Mapema wa Msumbiji aliyemaliza muda wake
hapa Tanzania
Bwana Zakaria Kupela alishauri rasilmali zilizopo kwa Mataifa yote mawili ni
vyema zikawekewa mikataba kwa faida ya Vizazi vijavyo.
Balozi Kupela alisema Mataifa yote mawili yamebarikiwa
kuwa na rasilmali nyingi mfano Maji,Madini, Gesi na Bahari ambazo kama hazikuwekewa utaratibu wa matumizi mazuri zinaweza
kuchukuliwa na wajanja.
Alifahamisha kwamba Kizazi kijacho kinaweza
kukumbwa na ushawishi wa Baadhi ya
Mataifa au mashirika ya Nje katika matumizi ya rasilmali hizo kinyume na haki ya Mataifa husika.
Alisisitiza suala la kuendelezwa utaratibu wa
kubadilishana Wanafunzi kati ya Tanzania
na Msumbiji ambao utasaidia zaidi uhusiano wa pande hizo.
Balozi Kupela ameelezea faraja yake kuona nyanja hiyo
imeshaleta matunda kwa vile tayari yapo mabadilishano ya wanafunzi 50 wa mwaka
wa pili sasa kati ya Tanzania
na Msumbiji.
Alisema mpango huo ukiandaliwa vyema unaweza pia kuratibu
mafunzo yatakayowawezesha Vijana wa pande zote mbili hizo kuelewa vyema kizazi
kilicholeta ukombozi kwa Mataifa hayo mawili.
Kuhusu suala la Amani Balozi Kupela aliwanasihi
Wananchi wa Zanzibar
kuendeleza amani waliyonayo ndani ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo hivi sasa ni darasa kwa mataifa
mengine Duniani.
Balozi Kupela alitahadharisha kwamba kitu chochote
chenye cheche ya kutenganisha jamii ni hatari kwa faifa ya kizazi kijacho.
Balozi Kupela alifika Ofisini kwa Balozi Seif kuaga rasmi
na kurejea Nyumbani Msumbiji baaada ya kumaliza muda wake wa Utumishi hapa Tanzania.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment