Viongozi mbali mbali wa kitaifa wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete leo wameshiriki katika hafla ya kuuaga mwili wa marehemu Bob Nyanga Makani iliyofanyika viwanja vya Kareem Jee jijini Dar es Salaam.
Viongozi wengine walioshiriki katika hafla hiyo ni pamoja Makamu wa Rais wa Jamhururi ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohd Gharib Bilal na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.
Bob Nyanga Makani aliyefariki dunia tarehe 9 mwezi huu kwa maradhi ya moyo, alikuwa ndiye Katibu Mkuu wa kwanza wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA na baadaye kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho.
Akisoma wasifu wa marehemu Bob Makani, Katibu Mkuu wa CHADEMA Dk. Wilbroad Slaa amesema marehemu aliwahi kushika nyadhifa mbali mbali serikalini zikiwemo Naibu Mwanasheria Mkuu nchini na Naibu Gavana wa Benki Kuu.
Amesema Chama chake kimepoteza mtu muhimu ambaye hata hivyo atakumbukwa kwa mazuri na mchango wake mkubwa kwa taifa.
Mwili wa marehemu Bob Makani ambaye ameacha vizuka na watoto saba umeagwa rasmi na kusafirishwa mkoani Shinyanga kwa ajili ya mazishi
Hassan Hamad (OMKR).

0 comments:

 
Top