Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameipongeza Serikali ya Cuba kwa uwamuzi wake wa kuendelea kusaidia kuiunga mkono Zanzibar katika masuala ya Huduma za Afya.
Pongezi hizo amezitoa hapo nyumbani kwake Mazizini wakati akizungumza na Madaktari Bingwa wa Cuba wanaotoa huduma za Afya Nchini baada ya kumaliza nao chakula cha pamoja cha usiku.
Balozi Seif Alisema Zanzibar hivi sasa imepiga hatua kubwa ya Maendeleo katika huduma za Afya ambapo Cuba ina mchango mkubwa na wa muda mrefu wa Utaalamu katika fani hiyo.
Alisema Afya ni miongoni mwa sekta ziliyopewa msukumo mkubwa na Serikali katika Sera ya kuwa na Kituo cha Afya kwa kila masafa ya Kilomita Tano Unguja na Pemba.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba sera hiyo inatarajiwa kwenda sambamba na mpango wa Wizara ya Afya wa Kuwapatia Taaluma Madaktari wazalendo 50 Chini ya Wataalamu wa Cuba.
“ Kundi hili la Madaktari 50 Wazalendo wanaofunzwa na Walimu wa Cuba litasaidia kupunguza uhaba wa Madaktari liliopo hapa Zanzibar”. Alisisitiza Balozi Seif Ali Iddi.
Aliowaomba Madaktari hao kujihisi kwamba huduma wanazozitoa zinafanana na zile walizokuwa wakizitoa Nchini kwao na Serikali itakuwa tayari kushirikiana nao ili lile lengo lao la kuwepo Zanzibar liweze kufanikiwa .
Naye Kiongozi wa Madaktari hao 16 Kutoka Nchini Cuba Dr. Freddy Fagindo alisema yeye na Timu yake wameelezea furaha yao kutokana na ukarimu mkubwa wanaoupata kutoka kwa Wananchi wa Zanzibar.
Dr. Freddy alimuhakikishai Balozi Seif kwamba Taaluma pamoja na huduma wanayoitoa itawafikia Walengwa ambao ni Wananchi walio wengi.
Kiongozi huyo wa Timu ya Madaktari wa Cuba ambae kituo chake kipo Mjini Dar es salaam alieleza kwamba Sera za Cuba ni kuona Taaluma iliyomo ndani ya Nchi hiyo inasambaa katika maeneo inayohitajia popote pale Duniani.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment