Wakati umefika kwa Vikundi vya Sanaa Nchini kuendelea kufanya kazi zao katika misingi ya Kibiashara ili kuwa na uwezo wa kujijengea mazingira ya kujitegema. 
Kazi ya sanaa si ya kuipuuza  wakati huu kwa vile  tayari imeshaonyesha muelekeo mpana wa kutoa ajira hasa kwa kundi kubwa la Vijana  katika sehemu mbali mbali Duniani. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo katika sherehe Maalum ya kutimia Miaka Mitano tokea kuasisiwa kwa Kikundi cha Taarab ya Kisasa Zanzibar { Zanzibar One Taarab } zilizofanyika katika Ukumbi wa Salama Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar. 
Sherehe hizo za aina yake zilizobeba wapenzi mashuhuri wa Muziki wa Taarab ya Kisasa { Modern Taarab } zilipambwa na wimbo mzito wa Mapenzi yangu pokea ulioghaniwa na Msanii Gwiji wa Sanaa ya Taarab Zanzibar ambae pia ni Mlezi wa Kikundi cha Zanzibar One Taarab Ustaadhi Mohd Ahmed. 
Akitoa nasaha zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  aliwapongeza Wasanii wa Kikundi hicho kwa juhudi zao za kutoa Burdani na kuwaomba waendelee kudumu na kuwa mahiri  zaidi.Alisema Vikundi vingi vya Sanaa huanzishwa vyema lakini hatma yake hufifia kutokana na migogoro lakini inapendeza kuona Zanzibar One Taarab bado inanawiri na kutamba. 
“ Kikundi chenu kina Wasani wazuri kama kungekuwa na tunzo naamini Kikundi hichi kingetokea mshindi. Kwa niaba yangu na Familia yangu nawapa  hongera kwa kutimia miaka mitano. Happy Birthday”. Balozi Seif alikifyagilia Kikundi hicho. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kwa vile Sanaa ni ajira mfano wa Wasanii wa Ulaya ipo haja kwa Washirika wa Fani hii kuendelea kuunga mkono Kikundi kama hicho ili Vijana hao wawe na uwezo kamili wa kuendesha Maisha yao. 
Katika kuunga mkono juhudi za kikundi cha Zanzibar One Taarab Balozi Seif ameahidi kukizawadia Shilingi 1,000,000/- Kikundi hicho ili zisaidia kutunisha mfuko wake. 
Akitoa shukrani kwa niaba ya Wasanii wenzake Mkurugenzi wa Kikundi hicho cha Zanzibar One Taarab Ustaadhi Abdulla Ali maarufu { Du  }  alisema lengo la kuanzishwa kwa Kikundi chao ni kutoa Burdani kwa Jamii kupitia Sanaa hiyo ya Taarab. 
Mkurugenzi Abdulla Du amewapongeza Viongozi na Washirika  wao wote walioamua  kujitolea kukisaidia Kikundi chao ambacho hivi sasa kiko katika muelekeo mzuri. 
Kikunci cha Zanzibar One Taarab kimeanzishwa Mwaka 2007 hivi sasa kikiwa na umri wa Mikaka Mitano. 
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top