Mataifa ya Bara la Afrika yanapaswa kushirikiana katika kuhakikisha matatizo ya upatikanaji wa huduma za mazji safi na salama kwa ajili ya Jamii za Mataifa hayo yanatanzuka.
Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohd Sheni wakati akiufungua Mkutano wa nne wa Siku tano wa Sera ya Maji Barani Afrika unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Kunduchi Beach Jijini Dar es salaam.
Dr. Sheni katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema yapop matatizo mengi yanayochangia ukosefu wa upatikanaji wa maji hali inayoendelea kusumbua Wananchi walio wengi hasa wale wa Vijijini.
Alisema ongezeko la Watu, harakati za Kilimo likiwemo lie la Mabadiliko ya hali ya hewa yanapelekea Mataifa mengi kushindwa kudhibiti matumizi bora ya huduma za maji.
Alifahamisha kwamba Viongozi, Taasisi za Kijamii , zile za Kiraia pamoja na Wananchi wanapaswa kuungana pamoja katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya Maji katika maeneo yao.
Alisisitiza kwamba Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kuhakikisha ifikapo mwaka 2015 iwe imeshapiga hatua kubwa ya kukabiliana na tatizo la upatikanaji wa maji safi.
Balozi Seif kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohd Sheni ameyapongeza Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya Elimu, Sayansi na Utamaduni { Unesco } na ile Taasisi ya Utafiti wa Maji ya Kimataifa { IHP } kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Mataifa ya Afrika katika kukabiliana na tatizo la Maji.
Alisema Mataifa mengi ya Bara la Afrika bado yanakabiliwa na ukosefu wa fedha pamoja na ufinyu wa Teknolojia ya Kisasa hali ambayo inafaa iondoke kwa kuungwa mkono na Mashirika hayo.
Akimkaribisha Balozi Seif WEaziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wa Serikali ya Tanzania Mh. Shukuru Kayambwa alisema utafiti unaendelea kufanywa na Wataalamu katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya maji unalenga kuwa na matumizi bora ya maji. Mh. Kayambwa alifahamisha kwamba huduma ya maji bado inaendelea kuwa muhimu kwa uhai wa Viumbe wakiongozwa na Mwanaadamu.
Mapema Mkurugenzi wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa { Unesco } kanda ya Afrika Profesa Joeoh massaquoi alisema Umoja wa Mataifa umeshaanza utafiti katika sekta ya Maji tokea mwaka 1975 ukiwa katika awamu sita.
Aliwapongeza Viongozi wa Bara l;a Afrika kwa uamuzi wao wa wa kutafuta mbinu za kukabiliana na tatizo hilo na kupanga mikakati ya kulinda rasilmali zilizomo barani humo ikiwemo ile muhimu wa Maji.
Mkutano huo wa nne unaofanyika Tanzania umeshirikisha wajumbe zaidi ya mia moja kutoka Nchi Tisa za Afrika wakiwemo pia Wataalamu wa Taasisi na Mashirika Hisani .Mikutano ya mwanzo ya Mataifa hayo imefanyika Nigeria mwaka 2006, Afrika Kusini mwaka 2008 na Nepal mwaka 2010.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top