1.0 Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa rehma zake za kutukutanisha hapa tukiwa wazima na afya njema na pia kwa kutuwezesha kufanikisha Mkutano huu wa Saba wa Baraza letu Tukufu. Shukurani zangu za dhati na Wajumbe wenzangu zikufikie wewe Mheshimiwa Spika pamoja na timu yako yote kwa kuendesha vikao vyetu kwa umahiri na umakini mkubwa. Pia, nawashukuru wale wote waliofanikisha mkutano huu wa saba kwa njia moja au nyengine; wakiwemo ndugu zetu mafundi mitambo pamoja na waandishi wa habari ambao muda wote wamekuwa nasi kufikisha majadiliano yetu ndani ya ukumbi huu, kwa wananchi wenzetu.
2.0 Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii adhimu kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohammed Shein kwa mashirikiano mazuri ambayo yalipelekea Rais Kikwete kuteua Tume ya Taifa ya Kuratibu Maoni na Mapendekezo ya Wananchi ya Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye wajumbe sawia kutoka pande mbili za Muungano; wajumbe 15 kutoka Zanzibar na wajumbe 15 kutoka Tanzania Bara. Wajumbe hawa 30 wameteuliwa kutoka tabaka mbali mbali za jamii yetu, wamo kutoka Vyama Vya Siasa, Jamii za Kiraia, Walemavu, Waandishi wa Habari na kadhalika. Kuteuliwa kwa Tume hii yenye Wajumbe wazito kumekidhi haja na matarajio ya wananchi wengi wanaosubiri kwa hamu kutoa maoni yao. Naomba uniruhusu niwapongeze kwa dhati kabisa wajumbe wote wa Tume hiyo na ninawatakia kazi njema yenye ufanisi ya majukumu iliyopewa.
Sisi Wawakilishi jukumu letu kwa sasa ni kuwaelimisha wananchi wetu kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao kwa uhuru bila ya woga wakati utakapowadia. Lakini ikumbukwe kuwa wakati huu ni muhimu sana kuvumiliana na kufuata taratibu zilizowekwa ili kutoa nafasi nzuri kwa kika mwananchi kuheshimu mawazo ya mwenzake na huu ndio msingi mzuri wa Demokrasia.
Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Mohammed Raza Hassan Dharamsi kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi kuwa Mwakilishi wa Jimbo la Uzini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi. Ni mategemeo ya wananchi wa Jimbo hilo kuvuna matunda bora baada ya kupanda mbegu bora. Mhe. Raza ni chuma cha pua, ni dhahiri sasa wananchi wa Uzini watapata maendeleo kwa haraka zaidi.
Aidha, napenda pia kuwapongeza Waheshimiwa wafuatao kwa kuteuliwa kushika nyadhifa mpya. Nampongeza Mheshimiwa Ali Juma Shamuhuna kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mheshimiwa Ramadhan Abdallah Shaaban kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Maji, Makaazi na Nishati, Mheshimiwa Abdillahi Jihad Hassan kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Suleiman Othman Nyanga kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo na Maliasili, Mheshimiwa Said Ali Mbarouk kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo na Mheshimiwa Mansour Yussuf Himid kwa kuteuliwa kuwa Waziri Asiyekuwa na Wizara Maalum. Nawaombea kwa Mwenezi Mungu awajaalie hekima na mafanikio makubwa katika nafasi zao. Wenzetu hawa wanamaliza Mkutano wa Saba wakiwa na nyadhifa tofauti na zile walizoanzia mkutano huu. Hongereni sana.
3.0 Mheshimiwa Spika, tumeanza mkutano huu wa saba bila ya mwenzetu, ambaye ametangulia mbele ya haki, Mheshimiwa Salum Amour Mtondoo, Mwakilishi wa Jimbo la Bububu kwa tiketi ya CCM. Mwenzetu huyu tutamkumbuka kwa uchapaji kazi wake bora. Alifuatilia kwa karibu matatizo ya Jimbo lake na alipenda sana kushirikiana na wenzake katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya nchi yetu. Kwa mara nyingine tena kwa niaba yangu na kwa niaba ya wajumbe wote wa Baraza lako tukufu napenda kutoa mkono wa pole kwa familia ya marehemu na sote kwa pamoja tumuombee mwenzetu makaazi mema peponi. Amin.
4.0 Mheshimiwa Spika, mkutano wetu huu wa saba umepata baraka ya kupokea na kujadili kwa kina Miswaada saba ya Sheria na hatimaye Waheshimiwa Wajumbe kwa busara zao wameipitisha miswaada hiyo. Miswaada hiyo ni kama ifuatayo:-
(i) Mswada wa Sheria ya Kufuta Sheria ya Ulipaji Mafao ya Viongozi wa Kitaifa Na. 4 ya Mwaka 1988 na Sheria ya Viongozi wa Kisiasa Nam. 6 ya Mwaka 1999 na kutunga Sheria Mpya ya Maslahi ya Mafao ya Viongozi wa Kisiasa baada ya Kustaafu Pamoja na Mambo Mengine yanayohusiana na Hayo.
(ii) Mswada wa Sheria ya Kufuta Sheria ya Tume ya Mipango Nam. 5 ya 1989 na Kutunga Sheria Mpya kwa ajili ya Uendeshaji wa Tume ya Mipango Zanzibar, Kazi zake, Uwezo wake na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.
(iii) Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo Zanzibar na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.
(iv) Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Utumishi wa Umma na mambo mengine yanayohusiana na hayo.
(v) Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Baraza la Mitihani la Zanzibar na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.
(vi) Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Utalii Nam. 6 ya 2009.
(vii) Mswada wa Sheria wa Kuanzisha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.
5.0 Mheshimiwa Spika, kutokana na kupitishwa kwa Sheria ya Tume ya Mipango, muundo wa tume hiyo unaendelea kutayarishwa kwa kuziunganisha Idara zote za Mipango, Sera na Utafiti kuwa chini ya usimamizi wa Tume ya Mipango. Aidha, Tume imo katika mchakato wa kuzifanyia mapitio kamati za mipango za mawizara mbali mbali ili kuhakikisha mipango ya Serikali inaenda sambamba kwa Serikali nzima.
6.0 Mheshimiwa Spika, Mswada wa Kamisheni ya Utalii ulipita kwa taabu kidogo hasa pale Wajumbe walipotofautiana kuhusu suala la ajira liwe kwa Mtanzania au Mzanzibari. Hii ndiyo demokrasia ilioonekana ndani ya Baraza letu ingawa hatimaye, Wajumbe waliotaka neno Mtanzania litumike ndani ya mswaada huu badala ya Mzanzibari wameshinda. Sina nia ya kurejesha mjadala huu lakini napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza Wajumbe wote waliosema ndio na wale waliosema hapana kwa kutumia haki yao ya kidemokrasia. Aidha, napenda kusema kuwa kuukubali Utanzania sio dhambi na wala sio usaliti wa Uzanzibari na kuukubali Uzanzibari sio dhambi na wala sio usaliti wa Utanzania. Naomba sana tusinyoosheane vidole kwa mambo haya. Tupimane uzalendo wetu kwa nchi yetu kwa vitendo vyetu. Tujiulize naisaidiaje nchi yangu kuendelea mbele? Nalipa kodi? Najiepusha na rushwa? Natumia madaraka yangu kwa maslahi ya nchi au kwa maslahi yangu? Nina hakika sote tunaipenda nchi yetu na tungependa kuona inaendelea vyema kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru sana Wajumbe wote wa Baraza lako tukufu, kwa kuipitisha Miswaada yote ambayo Serikali iliiwasilisha mbele yao. Naelewa wamefanya hivyo kwa lengo la kuipa nafasi Serikali yao kutekeleza mipango inayojipangia kwa ufanisi zaidi ili hatimaye tupige hatua ya maendeleo. Sasa kazi iliyo mbele yetu tushirikiane kwa pamoja katika kusimamia sheria hizi tulizozipitisha ili kukidhi matarajio ya wananchi wetu. Sheria isiyosimamiwa vizuri haiwezi ikatufikisha pale tunapotaka kufika. Zaidi ya hayo, tutakuwa tunakaribisha pole pole bila ya kujifahamu utawala wa mwenye nguvu mpishe badala ya utawala bora ambao msingi wake mkubwa ni watu wote ni sawa mbele ya sheria.
7.0 Mheshimiwa Spika, katika mkutano wetu huu wa saba mbali na Miswaada tuliyoijadili na kuipitisha, Baraza lako Tukufu pia lilipokea na kujadili Ripoti mbali mbali za Kamati za kudumu zikiwemo:
1. Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii;
2. Kamati ya Mifugo, Utalii, Uwezeshaji na Habari;
3. Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi;
4. Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala;
5. Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo;
6. Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa;
7. Kamati ya Kuchunguza na Kudhibiti Hesabu za Serikali na Mashirika (PAC); na
8. Kamati Teule ya Baraza la Wawakilishi.
Napenda kuwashukuru na kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati hizi pamoja na Wajumbe wao kwa kuandaa ripoti hizo nzuri zilizochunguza kwa kina mienendo ya Mawizara mbali mbali na Taasisi zao. Ripoti hizo zimesaidia sana kuitanabahisha Serikali katika mapungufu mbali mbali yaliyogundulika. Serikali itayazingatia kwa makini mapungufu yote yaliyogundulika kuchukuliwa hatua zifaazo kuyarekebisha au kuyaondoa kabisa mapungufu hayo. Na kwa kupitia Baraza hili Mhe. Spika nawaagiza Mawaziri wote kuzisimamia vyema wizara zao pamoja na Taasisi zilizo chini yao ili mapungufu hayo yasitokee tena.
8.0 Mheshimiwa Spika, Wajumbe wako pia walipata nafasi ya kupata Taarifa ya Hoja ya Eneo la Bahari la Ukanda wa Kiuchumi iliyotolewa na Mwanasheria Mkuu; Taarifa ya Mikopo ya Elimu ya Juu iliyotolewa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na Taarifa ya Hoja ya Ripoti ya Baraza la Manispaa ya Mji wa Zanzibar iliyowasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Aidha, Baraza lako Tukufu limepitisha marekebisho na mapendekezo ya kanuni za Baraza la Wawakilishi pamoja na kujadili hoja binafsi ya Mheshimiwa Hija Hassan Hija, Mwakilishi wa Kiwani kuhusu Ripoti ya Manispaa, Baraza imeona vyema liunde Kamati Teule yake ili ikafanye uchunguzi wake badala ya kujadili ripoti ambayo siyo yake. Kuhusu hoja binafsi ya Mhe. Hija, Baraza limeamua kuwa Kamati ya PAC ikafanye uchunguzi huo.
9.0 Mheshimiwa Spika, wakati wa kufunga Mkutano wa Sita wa Baraza lako Tukufu, nilizungumza kuhusu fedha zilizochangwa na wahisani na wananchi kwa ajili ya kuwasaidia wananchi walioathirika kutokana na ajali ya meli M.V Spice Islander 1. Nilisema Serikali itazigawa mara moja fedha zilizopatikana kwa wananchi walioathirika na ajali hiyo baada ya kumalizika zoezi la uhakiki wa majina ya wale wote wanaostahiki kulipwa na wale wananchi wenzetu waliofariki na wale waliookolewa wakiwa hai. Napenda kuliarifu Baraza lako tukufu na wananchi wote kuwa Serikali tayari imeshaanza ugawaji wa fedha hizo kwa kisiwa cha Unguja na linaendelea vizuri. Hadi kufikia tarehe 17 April, 2012 kati ya watu 457 waliofariki watu 256 sawa na asilimia 57 tayari wameshapatiwa fedha zao. Aidha jumla ya watu 122 waliookolewa sawa na asilimia 63 wameshalipwa fedha zao kati ya watu 193. Nawale ambao walihusika katika ajali ile na majina yao hayajajitokeza katika orodha ya malipo Serikali itayafanyia tathmini na wale wote waliohusika Serikali itawapatia haki zao. Baada ya kumalizika kwa zoezi hili hapa Unguja, zoezi litaanza rasmi kwa upande wa Pemba, nalo litafanyika baada ya muda si mrefu.
Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine tena, nachukua fursa hii adhim kuwapongeza sana wananchi kwa ustahamilivu na uvumilivu wao ambao umetusaidia sana kuendesha zoezi hili la uhakiki wa majina hadi kufikia hatua ambayo sasa tunalipa fedha tulizoahidi kwenye Baraza hili. Tunatoa wito pia kwa wananchi wote kufika katika vituo walivyopangiwa kwa kufuata utaratibu unaoendelea kutolewa kupitia vyombo vya habari hasa Shirika la Utangazaji la Zanzibar kupitia radio yake.
10.0 Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa bajeti katika kipindi cha mwezi Julai hadi Febuari 2011/2012 ni wa kuridhisha ingawa bado tumeendelea kuwa na changamoto katika upatikanaji wa rasilimali kutoka nje kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo. Katika kipindi hicho jumla ya Shilingi 340,969 milioni zimekusanywa sawa na asilimia 55.6 ya makadirio ya mwaka ya Tsh. 613,076 milioni. Aidha jumla ya matumizi katika kipindi hicho yamefikia Tsh. 296,766 milioni sawa na asilimia 69 ya makadirio ya mwaka.
11.0 Mheshimiwa Spika, zao la karafuu ni zao mama hapa kwetu Visiwani na litaendelea kuwa tegemeo la uchumi wetu kwa miaka mingi ijayo. Kwa bahati mbaya zao hili linakabiliwa na tatizo la ukongwe wa mikarafuu unaopelekea uzalishaji mdogo wa zao hili. Katika kutimiza azma ya kuimarisha zao la karafuu ili kuongeza uzalishaji na hatimaye kuongeza kipato cha wananchi na Taifa kwa jumla, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Maliasili inaendelea na kampeni ya upandaji mikarafuu katika maeneo yote husika ili kuutumia vyema msimu wa mvua zinazoendelea. Wizara ya Kilimo na Maliasili kupitia Idara ya Misitu na Maliasili zisizorejesheka imejiandaa kuhakikisha miche ya kutosha inapatikana katika vitalu vyake na kwamba wakulima wote nchini watapatiwa miche hiyo bila ya malipo. Nawaomba Waheshimiwa Wawakilishi wenzangu wanaotoka maeneo yanayolimwa karafuu kuichangamkia miche inayotolewa kwa kuwahamasisha wananchi katika majimbo yao kuipanda miche hiyo kwa wingi. Tunawaomba wakulima na wananchi wote kwa jumla kuitumia fursa hii adhimu kuzingatia maelekezo na masharti ya msingi yanayotolewa na wataalamu ikiwemo utayarishaji wa mashamba kabla ya kupatiwa miche hiyo.
12.0 Mheshimiwa Spika, kilimo cha Mpunga nacho kinaendelea vizuri msimu huu ikilinganishwa na msimu uliopita licha ya matatizo yaliyojitokeza ambayo yametokana na mabadiliko ya hali ya hewa. Takwimu zilizokusanywa na Wizara ya Kilimo na Maliasili zinaonyesha kwamba jumla ya eka 28,400 sawa na asilimia themanini na mbili (82%) ya lengo lililowekwa zimelimwa Unguja na Pemba hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2012 na kazi bado inaendelea. Hata hivyo, upatikanaji wa ruzuku ya pembejeo na huduma za utayarishaji wa mashamba haukuweza kuwafikia wakulima wote kama tulivyotarajia kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya wakulima waliohamasika na kujitokeza kutumia huduma hizo kulinganisha na uwezo uliokuwepo. Serikali itaendelea kufikisha huduma hizo kwa wakulima wengi kadri itakavyowezekana katika misimu ijayo ili waweze kuongeza uzalishaji na hatimae kujiongezea chakula na kipato chao na Taifa kwa jumla. Aidha, Serikali inawaomba wakulima kuzingatia ushauri unaotolewa mara kwa mara na wataalamu wetu wa kilimo kupitia vyombo vya habari, ikiwemo matumizi ya mbegu bora na kulima kwa kuzingatia mabadiliko ya miongo ya mvua ili waweze kuepuka hasara zilizojitokeza katika baadhi ya maeneo msimu uliopita.
13.0 Mheshimiwa Spika, sekta ya mawasiliano ni muhimu sana kwa maendeleo ya uchumi wa nchi yetu. Mipango ya Serikali yetu ya kuunganisha miji na vijiji kwa mtandao wa barabara itaendelea kutekelezwa kwa kasi zaidi Unguja na Pemba. Katika kikao kilichopita cha Baraza letu nilizungumzia barabara ya Mfenesini – Bumbwini yenye urefu wa kilomita 13.2 kuwa iko katika hatua za kukamilika. Napenda kulijulisha Baraza lako Tukufu kuwa barabara hii imekamilika sasa pamoja na madaraja ya Mwanakombo, Tingatinga na Mto wa Maji. Kukamilika kwa barabara hii pamoja na madaraja niliyoyataja kunategemewa kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi ikiwemo usafirishaji wa bidhaa kwenda kwenye masoko kwa urahisi zaidi pamoja na kufungua maeneo yetu kwa wawekezaji wa ndani na nje. Nawaomba wananchi wanaoishi sehemu ambazo madaraja hayo yamejengwa kuwa walinzi dhidi ya uharibifu wa aina yoyote ile ili yaendelee kutuhudumia kwa miaka mingi ijayo kama tulivyokusudia. Aidha, nawaomba madereva wanaotumia madaraja haya kuwa waangalifu kwani uzoefu wetu unaonyesha kuwa ajali nyingi za barabarani Mkoa wa Kaskazini hutokea mara kwa mara sehemu zenye madaraja. Nawaomba sana wadereva hao waepuke ajali hizo kwa kufuata sheria za barabarani.
14.0 Mheshimiwa Spika, Serikali yetu kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo hivi karibuni imekarabati mtambo wa mawimbi mafupi (short waves) uliopo Dole kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China. Mtambo huo umekabidhiwa kwa Serikali tarehe 9 Machi, 2012. Kukarabatiwa kwa mtambo huo kunafanya matangazo ya redio ya Shirika la Utangazaji (ZBC) kusikika hadi nchi za Mashariki ya Kati.
Wizara pia inaendelea na ujenzi wa studio na ofisi katika eneo la Bungi pamoja na nyumba mbili za kisasa za wafanyakazi zinazojengwa kwa lengo la kuimarisha utendaji mzuri wa kazi. Studio imehamishiwa Bungi kutoka Chumbuni kwa sababu za usalama wa ndege uliokuwa ukihatarishwa na mnara uliokuwepo huko.
15.0 Mheshimiwa Spika, sekta ya Utalii itaendelea kuwa tegemeo la uchumi wa nchi yetu na ndio maana Serikali yetu kila inapoona kuna haja ya kujenga mazingira mazuri kwa lengo la kuimarisha sekta hiyo huwa inafanya hivyo. Marekebisho ya Sheria namba 6 ya Mwaka 2009 na Mswaada wake kupitishwa na Wajumbe wa Baraza lako Tukufu katika mkutano huu ni hatua muhimu kuelekea kwenye utalii utakaosaidia juhudi zetu za kujenga maisha mazuri kwa wananchi wetu. Kamisheni yetu ya Utalii katika jitihada zake za kuimarisha Utalii nchini kwa njia ya kuitangaza Zanzibar katika nchi mbali mbali duniani imepata mafanikio mazuri. Hivi karibuni Zanzibar imepata tunzo ijulikanayo “The Annual Russian Tourism Award” kwa kuwa kituo bora cha utalii barani Afrika. Tunaipongeza Kamisheni yetu ya Utalii kwa mafanikio haya makubwa na tunawaomba waendelee na jitihada zao za kuitangaza Zanzibar duniani kote. Hata hivyo, ni vyema ikaeleweka kuwa kazi ya kuitangaza Zanzibar ni kazi yetu sote. Wengi wetu Barazani hapa tunapata fursa ya kutembelea nchi tofauti duniani. Tutumie basi fursa kama hizo kuitangaza nchi yetu kwa watu tunaokutana nao.
16.0 Mheshimiwa Spika, Taifa letu linatambua haki za walemavu. Watu wenye ulemavu wana haki na fursa sawa kwa wote. Si vyema kwa jamii yetu kuendelea na tabia ya kuwanyanyasa na kuwadhalilisha watu wenye ulemavu. Taasisi nyingi za Serikali hivi sasa zinajenga majengo mapya. Natoa wito kwa wale wote wanaojenga majengo kwa ajili ya kutoa huduma za umma, kuhakikisha kwamba majengo hayo yanakuwa rafiki kwa watu wenye ulemavu. Kuwa rafiki maana yake mlemavu aweze kutumia jengo hilo kama watu wengine, kwa kuwekewa miundombinu ambayo itamrahisishia kuingia ndani ya jengo hilo na kutumia fursa zilizomo ndani yake. Kwa mfano, majengo hayo yanatakiwa kuweka vyoo maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu katika ghorofa zote za jengo na pia mlemavu apate fursa ya kwenda ofisi yoyote ndani ya jengo hilo bila ya vikwazo. Suala la ajira kwa watu wenye ulemavu wenye sifa na uwezo ni la umuhimu pia. Waajiri wasiwanyime fursa watu hawa kwa sababu tu ya ulemavu wao, ni muhimu kuangalia sifa na uwezo wao na kuwapa vipaumbele. Ubaguzi mzuri (Positive discrimination) wakati mwengine inafaa kutumika katika jamii kwa lengo la kuwanyanyua wale walioachwa nyuma. Kwa hivyo suala la kuwapa vipaumbele walemavu wakati wa ajira ni muhimu sana.
17.0 Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetayarisha Sera ya Mifugo ambayo imeweka mazingira mazuri na mikakati endelevu ya kuendeleza sekta ya mifugo. Sera ya sasa imezingatia mambo muhimu ya kuiendeleza sekta hiyo ambayo hayakuwemo katika sera iliyokuwepo. Mambo yaliyokuwemo katika sera ya sasa ni pamoja na mambo ya utafiti, ustawi wa wanyama, uzalishaji na utumiaji wa nishati itokanayo na samadi, kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na mifugo, kuendeleza uzalishaji wa ndani na upatikanaji mitaji ya fedha kwa wajasiriamali. Sera hii tunategemea itakuwa kichocheo cha ufugaji bora nchini.
18.0 Mheshimiwa Spika, nchi yetu ilikumbwa na uhaba wa mchele wiki za mwanzo wa mwezi wa Machi, 2012, hali ambayo ilisababisha bei ya mchele kupanda kutoka shilingi 50,000/= kwa kipolo cha kilo 50 mpaka shilingi 57,000/=. Hali hii ilisababishwa na kuchelewa kufika kwa mchele ulioagizwa mwishoni mwa mwezi wa Machi, 2012. Hata hivyo, tayari mchele umeanza kuingia kutoka nje ambapo kiasi cha tani 12,251 zimeingia mapema mwezi huu. Mchele huo unatarajiwa kutumika kwa miezi miwili, matumizi kwa mwezi yanakisiwa kuwa ni tani 6,000. Kwa upande wa bei hivi sasa imeshuka na mchele unapatikana kwa shilingi 52,000/= kwa kipolo cha kilo 50. Tunawasihi wafanya biashara kuacha tabia ya kuutorosha mchele wetu kimagendo kwa sababu ya kushuka kwake kwa bei.
19.0 Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Afya inatarajia kuanzisha kampeni ya Kitaifa ya kutoa dawa za Kichocho na Minyoo kwa Wananchi kuanzia tarehe 28 mwezi huu wa Aprili. Madhumuni ya kampeni hii ni kupambana na maradhi ya Kichocho na Minyoo ambayo yamekuwa yakisumbua Wananchi wengi hasa watoto katika visiwa vyetu vya Unguja na Pemba.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa za kitaalamu maradhi ya kichocho yameenea kwa asilimia 15 kwa kisiwa cha Pemba na asilimia 8 kwa kisiwa cha Unguja. Hii ina maana maradhi ya kichocho yapo katika Visiwa vyetu vya Unguja na Pemba. Na kwa Unguja maradhi yamesambaa zaidi katika Mkoa wa Kaskazini. Serikali kupitia Wizara ya Afya imekuwa ikichukuwa jitihada mbali mbali kutokomeza kichocho na minyoo ambapo kampeni hii ni mojawapo ya juhudi hizo.
Mheshimiwa Spika, dawa hizi ni za kuzuia wadudu wa kichocho na kuua minyoo iliyokuwemo mwilini, Dawa hizi hazina matatizo kwa afya ya binaadamu na Serikali imeamua kuzitoa dawa hizi bure. Hivyo natoa wito kwa wananchi wote kutokua na hofu juu ya madhara ya dawa hizi. Nawaomba Wawakilishi wenzangu kushajiisha na kuwaelimisha wananchi kula dawa. Narejea tena dawa hizi hazina matatizo kwa afya ya binaadamu tuzitumieni ili lengo la Serikali yetu la kutokomeza kabisa kichocho nchini ifikapo 2015 lifanikiwe.
20.0 Mheshimiwa Spika, kama tujuavyo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimo katika maandalizi ya Sensa ya Watu na Makaazi ambayo imepangwa kufanyika nchini kote kuanzia Jumapili ya tarehe 26 Agosti mwaka huu, Taarifa zitakazokusanywa katika Sensa ya mwaka 2012 zitatumika kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2020 kwa Zanzibar, Mkakati wa Kukuza na Kupunguza Umaskini Zanzibar – MKUZA. Takwimu hizo zitatumika pia kutathmini utekelezaji wa malengo ya Milenia ifikapo mwaka 2015.
Mheshimiwa Spika, kauli mbiu ya Sensa ya safari hii ni “Sensa kwa Maendeleo ya Taifa: Jiandae kuhesabiwa”. Kauli mbiu hii tuifanyie kazi sote kwa pamoja, Viongozi na wananchi tunaowaongoza katika kufanikisha sensa ya safari hii. Maelezo mengi yametolewa kuhusu umuhimu wa sensa kwa maendeleo yetu. Kwa kifupi sensa inatueleza sisi ni nani na kwa namna gani tumebadilika kwa kipindi kilichopita. Takwimu za sensa zinasaidia sana Serikali kupanga mipango yake kwa kuelewa vyema mahitaji ya wananchi wake. Takwimu hizi pia zitatusaidia katika kushajiisha uwekezaji katika nchi yetu. Takwimu sahihi za idadi ya watu, hali ya uchumi wa nchi kwa jumla ni miongoni mwa taarifa muhimu kwa muwekezaji. Kwa rafiki zangu wafanyabiashara, takwimu za sensa zitawasaidia wapi katika nchi wafungue biashara zao. Sisi Wanasiasa pia takwimu hizi za sensa zitatusaidia kuelewa wapiga kura wengi tutawapata vijiji vipi! Takwimu za sensa tutakazozipata baada ya sensa hii ni mali kwa kila mwananchi, inategemea tutazitumia vipi. Maelezo mengi kuhusu Sensa hii tumeshayapata kupitia Semina mbili tulizofanyiwa na Wataalamu wetu wa Sensa. Ni matumaini yangu kwamba yale yote tuliyoelezwa katika semina hizo tutayafanyia kazi ipasavyo.
21.0 Mheshimiwa Spika, jukumu la kila Kiongozi kuanzia chini hadi juu kuelekeza uongozi wake wa busara katika kufanikisha sensa ya mwaka huu na jukumu la mwananchi kuanzia sasa kuhakikisha kuwa siku ya Sensa inapowadia anakuwa mstari wa mbele katika kuhesabiwa. Natoa wito kwa Makampuni mbali mbali nchini yajitokeze kusaidia kuhamasisha sensa ya mwaka huu. Milango iko wazi Makampuni hayo kushirikiana na Kamati ya Taifa ya Sensa katika kuhamasisha wananchi kwa vipeperushi au hata kuchapisha fulana na mambo kama hayo.
22.0 Mheshimiwa Spika, sote ni mashahidi nchi yetu iko katika hali ya kupigiwa mfano wa Amani na Utulivu na hasa baada ya Kuundwa kwa Serikali ya Mapinduzi yenye Mfumo wa Umoja wa Kitaifa. Matumaini ya wananchi wetu, hali hii itabakia na itaendelea kwa kizazi kilichopo na kijacho. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa upande wake imedhamiria kwa dhati kudumisha hali hii ya amani na utulivu Visiwani mwetu. Kurasa zetu za historia ambazo zilijaa migogoro ya kisiasa, uhasama na hali ya kutoaminiana, tumezitia moto; kurasa tulizonazo tunaandikia historia yetu mpya, kichwa chake cha habari kinasomeka; Umoja, Amani na Utulivu. Ndani ya kurasa hizo habari tunazozinakili na ambazo zimetawala ni maendeleo kwa wote; haki kwa wote; maji safi kwa wote; elimu bora kwa wote, afya njema kwa wote na kadhalika. Hakuna mwenye ubavu kubadilisha kichwa hiki cha habari kwani wenyewe tupo macho. Pia hakuna mwenye ubavu kubadilisha yale tunayoyanakili kwenye kurasa hizi kwani wenyewe tupo, kuangalia.
23.0 Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kumetokea kikundi cha wenzetu wachache kinachoendesha makongamano na mihadhara inayotishia hali yetu ya amani na utulivu niliyoielezea. Kikundi hiki mbali na kuhamasisha kwa nguvu watu kuukataa Muungano pia kinatukana kwa nguvu Viongozi wetu na wale wanaounga mkono Muungano.
Mheshimiwa Spika, Serikali haikatazi kikundi chochote kuendesha mihadhara au makongamano nchini na ndio maana tumevumilia tukidhani kuwa nia ya mihadhara hiyo ni kuelimisha jamii, lakini mihadhara hiyo imebadilika sura na badala ya kuelimisha imekuwa ni uwanja wa kashfa, kejeli na matusi tena matusi mengine ni ya nguoni kwa Viongozi wetu, jambo ambalo ni kinyume kabisa na utamaduni wa mzanzibari na misingi ya kidemokrasia.
Mheshimiwa Spika, napenda ieleweke wazi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitakivumilia kikundi chochote kitakachoonekana kuhatarisha amani, utulivu na umoja wa wananchi wetu. Hatuko tayari kurudishwa kule tulikotoka ambako tukiishi kwa chuki na uhasama mkubwa. Hatutasita kukizuwia kikundi chochote kile kuendesha mihadhara au makongamano tutakayobaini yanahatarisha usalama wa nchi yetu. Kwa hili hatutokuwa na muhali na mtu yoyote yule.
Mheshimiwa Spika, ninawaomba sana Wtanzania wenzangu kuwa fursa iliyotolewa na Serikali zetu kwa kuleta mchakato wa katiba mpya ni jambo la kihistoria na linaloonesha kukuwa kwa demokrasia katika nchi yetu. Hivyo litakuwa ni jambo la busara sana kutumia fursa hii kwa mustakabali wa nchi yetu badala ya baadhi ya wenzetu kujitokeza kuharibu dhamira njema ya Serikali.
24.0 Mwisho, Mheshimiwa Spika, kwa mara nyengine tena napenda kukushukuru wewe binafsi na kwa kupitia kwako kwa Naibu Spika na Wenyeviti wetu wa Baraza la Wawakilishi kwa namna mlivyouendesha mkutano huu kwa busara na utulivu mkubwa. Mkutano huu ulijaa hekima, maarifa na uvumilivu mkubwa. Hivyo, napenda niwapongeze Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza kwa michango yao mizuri iliyokuwa ya faida kubwa kwa Serikali. Hii imeonyesha uwezo wao wa kuisimamia na kuielekeza Serikali vizuri. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeithamini sana michango hiyo na naahidi Serikali itachukua hatua kwa yale yote ambayo Wajumbe wameyaelekeza.
25.0 Mheshimiwa Spika, kuhusu taarifa ya Kamati Teule ambayo imewasilishwa katika Baraza lako Tukufu na kuchangiwa na Waheshimiwa Wajumbe kadhaa wa Baraza lako tukufu. Kwa niaba ya Serikali nachukua fursa hii kuipongeza sana kazi iliyofanywa na Kamati hiyo pamoja na michango yote iliyotolewa kuhusiana na ripoti hii.Ripoti ya Kamati Teule imetupa nafasi nyengine kama Serikali kuona namna ambavyo Baraza la Wawakilishi katika Awamu ya Saba ya Serikali ya Zanzibar imejipanga kuona kuwa Serikali inabadilika katika utendaji wake na uwajibikaji wake.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini juhudi hizi za Baraza la Wawakilishi kwa sababu zimeunga mkono kauli mbiu ya Serikali ya Awamu ya Saba kuwa tunaachana na utendaji wa kimazoea (Business as usual).
Mheshimiwa Spika, mara zote Mhe. Rais wa Zanzibar anakuwa akisema “Tushirikiane kupambana na rushwa, wizi na ubadhirifu wa mali ya umma kwa lengo la kujenga Taifa lenye kufuata Utawala Bora, usawa na Haki za Binadamu”. Lazima sote ndani ya Serikali tuuheshimu msemo huu wa Rais wetu.
Mheshimiwa Spika, Serikali inachukulia taarifa ya Kamati Teule (miongoni mwa Kamati nyengine za Baraza) kuwa ni mchango thabiti wa Baraza katika kuunga mkono juhudi na mwelekeo wa Serikali ya Zanzibar ya Awamu hii. Serikali kuu imetoa mwelekeo, Baraza la Wawakilishi limetoa mfano mzuri juu ya mwelekeo huo. Sasa nijukumu la Watendaji wa Serikali katika ngazi zote kufuata nyayo, na tunakiri kuwa ni jukumu la Uongzi wa juu wa Serikali kulisimamia jambo hili.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeyasikia vizuri maelezo yaliyomo kwenye taarifa ya Kamati pamoja na michango mizuri ya Wajumbe wa Baraza. Nataka kulihakikishia Baraza lako Tukufu kwamba Serikali nayo itakuwa makini sana katika kuifanyia kazi kwa vitendo Taarifa ya Kamati Teule.
26.0 Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa nawatakia Wajumbe wote safari njema ya kurejea Majimboni kwao ili wakaungane na wananchi wao kuendeleza harakati zao za kuyaletea Majimbo yao maendeleo.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naomba kutoa hoja ya  kuliahirisha Baraza lako Tukufu hadi Jumatano tarehe 13 Juni, 2012 saa 3.00 asubuhi.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja

0 comments:

 
Top