Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar , Maalim Seif Sharif Hamad amewataka viongozi wa Shirika la Umeme, Idara ya Mazingira na Polisi kudhibiti vitendo vya baadhi ya wananchi kuchimba mchanga maeneo yenye nguzo za umeme mzito, ili kuepusha hatari ya kukosekana umeme au kutokea maafa.
Makamu wa Kwanza wa Rais aliyasema hayo wakati alipotembelea eneo la Kwarara, Wilaya ya Magharibi Unguja kujionea athari kubwa zilizosababishwa na vitendo vya uchimbaji wa mchanga chini ya nguzo za umeme mzito unaopokelewa kutoka kituo cha Fumba.
Alisema iwapo vitendo hivyo havitadhibitiwa kuna hatari nguzo hizo zikaanguka kabisa na kusababisha Zanzibar kukosa umeme kwa kipindi kirefu, lakini pia vinaweza kusababisha maafa, iwapo nguzo ya umeme mzito itaanguka.
Makamu wa Kwanza wa Rais alisema taasisi hizo pamoja na Wilaya ya Magharibi hazina budi kulifanyia tathmini ya kina tatizo la uchimbaji wa mchanga chini ya nyaya hizo, katika kipindi cha wiki mbili na baadaye kuchukua hatua zinazofaa kukomesha tabia hiyo.
Alisema sheria za Mazingira pamoja na kanuni za miji ziko wazi, hivyo wale wanaothibitika kujihusisha na uchimbaji wa mchanga bila ya kufuata sheria, wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria zilizopo.
Akitoa maelezo kwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Sheha wa Shehia ya Kwarara, Haji Pandu Jecha alisema pamoja na uongozi wa Shehia kuwachukulia hatua baadhi ya wananchi waliokamatwa wakichimba mchanga katika maeneo hayo, bado vitendo hivyo vinaendelea kwa kasi.
Alisema hivi sasa watatumia ulinzi shirikishi chini ya utaratibu wa polisi jamii, kukomesha vitendo vya uchimbaji wa mchanga vinavyofanywa chini ya nguzo hizo zinazosafirisha umeme kutoka Gridi ya Taifa, ambapo wahusika huchimba mchanga huo nyakati za usiku.
Meneja Operesheni wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Abdalla Haji Steni alisema vitendo vya uchimbaji mchanga chini ya nguzo nyingi za umeme vinaendelea kwa kasi kubwa, licha ya kuwa na madhara makubwa kwa nchi.
Alieleza kwamba katika kufanikisha maagizo yaliyotolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Shirika la Umeme litashirikiana na wadau wengine kufanikisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuzilinda nguzo hizo zisiathiriwe.
Hassan Hamad (OMKR)
0 comments:
Post a Comment