Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amekabidhi mchango wa Shilingi Milioni Moja { 1,000,000/- } kwa ajili ya uendelezaji wa Ujenzi wa Jengo jipya la Skuli ya Sekondari ya Masista iliyopo Mitundu Mkoani Singida.
Mchango huo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa alipotembelea Ujenzi wa Jengo hilo wakati wa ziara yake ya siku tatu Mkoani Singida ya tarehe 7 February mwaka 2012 akiwa Mlezi wa Mkoa huo Kichama.
Balozi Seif amekabidhi Mchango huo kwa Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki Mh. Dianna Chilolo hapo katika Ofisi ya watu Mashuhuri { VIP } iliyopo katika jengo la Karimjee Mjini Dar es salaam.
Akitoa mchango huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema amelazimika kutoa mchango huo kutokana na uamuzi wa Uongozi wa Skuli hiyo kutoa upendeleo wa kuwapatia Elimu bila ya ada Watoto Yatima na wale wanaoishi katika Familia zenye mazingira magumu.
Akipokea Mchango huo Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki Mh. Dianna Chilolo amempongeza Balozi Seif kwa Jitihada zake za kuunga mkono Maendeleo ya Elimu Mkoani Singida.
Alisema Mchango huo ni moja ya Vitendo vinavyoendelea kuwapa moyo Wananchi wa Singida katika harakati zao za kupewa msukumo wa Kimaendeleo wakati wanapoanzisha Miradi ya Utawi wa Jamii.
Mh. Dianna Chilolo ameahidi kwamba mchango alioutoa Balozi Seif ataufikisha kwa wakati muwafaka na kutumiwa kwa lengo lililokusudia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliutembelea Mkoa wa Singida mnamo Mwezi wa Pili mwaka huu katika ziara ya siku tatu akiwa mlezi wa Mkoa huo Kichama.
Balozi Seif katika ziara hiyo alibahatika kuweka Mawe ya Msingi pamoja na kuzindua miradi tofauti ya Maendeleo na Kiuchumi ya Wananchi wa Singida ikiwemo pia ile ya Chama Cha Mapinduzi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top