Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alisema jitihada za Walimu wa Madrasa Nchini katika Kuwafinyanga vyema Watoto kuelekea kwenye elimu wa Dini zinafaa kuungwa mkono na Wazazi wote Nchini.
Mama Asha alieleza hayo baada ya kushuhudia Vipaji vya Wanafunzi wa Almadrasatil Nnajia Al- Islamia Lkarim iliyopo Mtaa wa Muungano katika hafla ya Tathmini ya Maendeleo ya Wanafunzi wa Madrasa hiyo.
Mama Asha alisema Ushiriki wa karibu wa Wazazi katika kufuatilia Maendeleo ya Watoto wao ndani ya Madrasa huwawezesha Walimu wao kuwa na moyo zaidi wa kufikisha Taaluma zaidi kwa Watoto hao.
“ Raha ya Mzazi kumuona Mtoto wake anafanya vyema katika masomo yake isiishie wakati wa sherehe na zawadi tuu bali ianzie kwenye ushiriki wa pamoja wa ufinyazi wa mtoto huyo” Alisisitiza Mama Asha.
Mama Asha alielezea umuhimu wa Wazazi kuwekeza zaidi kwa kuchangia Sekta ya Elimu kwa lengo la kuwa na Taifa la Wasomi wa Elimu zote Mbili.
Alikemea Tabia ya Baadhi ya Watu wakiwemo pia Walimu wa Madrasa kuwamua kufunga ndoa na Wanafunzi ambao bado hawajamaliza masomo yao kwa kisingizio cha kuchaguwa watoto wenye Tabia nzuri.
Alisema kufanya hivyo mbali ya kuondosha uaminifu kwa Jamii inayowazunguuka lakini pia inachangia kudumaza kwa kiwango cha Elimu ambacho tayari kimeshajichomoza kwa watoto hao.
Katika Risala yao Wanafunzi hao wa Almadrasatil Nnajia Al- Islamia Lkarim wameelezea changa moto wanazokabiliana nazo Chuoni hapo kuwa ni pamoja na Udogo wa Jengowa Jengo la Kusomea , uhaba wa Misahafu, likiwemo pia muda wa Tuition unaoingiliana na Mafunzo ya Dini.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi katika kuunga mkono juhudi za Madrasa hiyo kujipatia jengo kubwa zaidi amehamasika kuchangia Shilingi Milioni Moja kuongezea fedha kwa ajili ya ununuzi wa nyumba itakayokuwa Jengo la madrasa hiyo.
Katika hafla hiyo pia Mama Asha alitoa zawadi kwa Wanafunzi sita waliofanya vizuri katika masomo yao pamoja na wale walioonyesha Heshima na adabu nzuri zaidi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top