Chama cha Mapinduzi kitaendelea kuheshimika ndani ya Jamii endapo Viongozi wanaokisimamia kuanzia ngazi ya Shina hadi Taifa watatekeleza vyema wajibu wao kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2010.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akifungua kikao cha Baraza la Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa Mjini Magharibi uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Grand Palace Malindi Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema huu si wakati wa kutomuonea haya Mtu ye yote anayeendeleza tabia za kudhoofisha Chama ambae hujihisi kwamba madaraka aliyopewa na Wanachama ni yake Binafsi.Aliwaomba Vijana hao wa CCM kuwakaba Viongozi wasiotaka kutekeleza majukumu yao ndani ya Matawi na Majimbo yao kwa lengo la kukisafisha Chama hicho ili kiendelee kuwa kimbilio la Wanyonge.
“ Chaguzi hizi zinazoanza ndani ya Chama ni vyema zikawa chanzo cha kusafisha Chama kwa kuwaacha watu wenye sura mbili katika Uongozi”. Alitanabahisha Balozi Seif.
Akizungumzia Utekelezaji wa Ilani ya Chama ya Mwaka 2010 ndani ya Serikali Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali itahakikisha kwamba wale wanaokwenda kinyume na azma ya Serikali pamoja na Ilani hiyo wanachukuliwa hatua. Alisema lengo la Serikali ni kuwapatia huduma bora wananchi kwa Mujibu wa Sheria na Taratibu zilizowekwa.
“ Tumekubali kuwa na Mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa nia ya kutandika Demokrasia makini ndani ya Jamii kupitia Ilani iliyoridhiwa na Wapiga kura . Hivyo Mtendaji asiyekubali mfumo huo ni vyema akajiondoa mwenyewe Madarakani” Alionya Balozi Seif.
Mapema Katika Taarifa yao iliyosomwa na Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa Mjini Magharibi Ndugu Mgeni Mussa Vijana hao walisema Serikali inapaswa kuwatenga Watendaji wasiotaka kufuata Ilani ya Chama ya mwaka 2010 katika utekelezaji wa Majukumu waliyopangiwa na Taifa.
Vijana hao pia wameipongea Serikali Kuu kupitia Kamati ya Maafa Zanzibar kwa umakini wake katika harakati za uokozi kwenye janga la Kuzama kwa Meli ya M.V Spice Islanders mwezi Septemba mwaka 2011.
Kikao hicho cha Baraza la Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa Mjini Magharibi kiliambatana pia na Semina iliyojumuisha mada mbili ambazo ni Uwezo wa Vijana ndani ya Chama cha Mapinduzi pamoja na Mchakato wa kuelekea kwenye Katiba Mpya ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Balozi Seif akiwa pia Mbunge wa Jimbo la Kitope amekabidhi Mabati Mia moja na Ishirini pamoja na vifaa vyake vyote vya kuezekea kwa ajili ya Tawi la Chama Cha Mapinduzi la Kitope A vikiwa na gharama ya Shilingi milioni tano.
Akimkabidhi Mwenyekiti wa CCM Tawi la Kitope A Ndugu Mikidadi Adam Mbunge huyo wa Kitope amewapongeza Wanachama wa Tawi hilo kwa uwamuzi wao wa Kujenga Tawi lenye hadhi ya Chama chao.
Baadaye Balozi Seif akakabidhi Mabati Mia Mbili na Thalathini na Mbili yenye thamani ya Shilingi Milioni Nne kwa ajili ya kusaidia nguvu za Wizara ya Elimu Kuliezeka Jengo Jipya la itakayokuwa Skuli ya Msingi ya Matetema iliyopo Kazole.
Mabati hayo amemkabidhi Sheha wa Shehia ya Matetema Bwana Mohd Bakar Mohd na kusema kitendo cha Wananchi hao cha kuwapunguzia masafa marefu watoto wao kutafuta Elimu kinafaa kuigwa na Maeneo mengine.
Jengo hilo la Skluli ya Matetema lenye madarasa manne, Ofisi ya mwalimu Mkuu na Stoo linatarajiwa kuezekwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar muda si mrefu.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top