Wazazi na walezi Nchini wamehimizwa kujenga tabia ya kuwapeleka watoto wao katika Vituo vya Maandalizi kwa lengo la kuwajengea mazingira bora ya kielimu hapo baadaye.
Himizo hilo limetolewa na Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi kwenye Mahfali ya Tatu ya Kituo cha Maandalizi cha Dhin-Noorayni kiliopo Fujoni ndani ya Jimbo la Kitope.Mama Asha alisema mazingira hayo muhimu yatasaidia kuwawezesha Watoto hao kuwa makini na mahiri wakati watakapoanza mafunzo yao ya Elimu ya Msingi.
“ Mtakapoanza mapema mfumo huu muelewe kwamba tayari mtakuwa mmeshatekeleza ile Sera ya Elimu ya kuhakikisha Mtoto ye yote anapatiwa kwanza elimu ya Maandalizi kabla ya kujiunga na Skuli ya Msingi ”. alisisitiza Mama Asha Suleiman Iddi.Amewapongeza Wazazi na walezi kwa juhudui zao za kusaidiana katika malezi ya pamoja ya Watoto wao. Mama Asha amechangia Shilingi Laki 500,000/- na kuahidi kutoa fedha kwa ajili ya Matofali ya Kumalizia Ujenzi wa Kituo hicho cha Maadalizi Fujoni.
Akizungumzia suala la Mitihani ya Darasa la Kumi na Mbili yaani { Form IV } ya mwaka 2011 Mama Asha alielezea kusikitishwa kwake na matokeo mabaya ya Skuli ya Fujoni ambayo ilikuwa ikifanya vyema katika miaka ya nyuma.
“ Nimejisikia kuwa mwenye huzuni baada ya kupata matokeo hayo na kufahamu ni mwanafunzi mmoja tuu aliyebahatika kuendelea na masono yake ”. Alisikitika Mama Asha.
Mama Asha ameuagiza Uongozi wa Skuli ya Fujoni,Wazazi na Walezi wa Wanafunzi kukaa pamoja na kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo lililopelekea kushuka kwa kiwango cha Ufaulu cha Wanafunzi wa Skuli hiyo.
Akisoma Taarifa fupi Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Kituo hicho cha Maandalizi cha Dhin-Noorayni Mwalimu Hawana Abdulla alisema lengo la kuanzishwa kwa kituo hicho ni kuwapunguzia masafa marefu watoto wa Kijiji hicho.
Mwalimu Hawana alisema Kituo chao kimepiga hatua kubwa kwa kutumia mbinu bora za kufundishia ziliyopelekea kuongezea kwa idadi kubwa ya Wanafunzi Kituoni hapo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top