Wananchi walio wengi wa Zanzibar wanaendelea kujivunia mwamvuli wa baraka ya hali nzuri ya Kisiasa Zanzibar ambayo wako tayari kuiimarisha ili kuwa bora zaidi hapo baadaye. Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akiufunga Mkutano wa Pili wa siku mbili wa Hali ya Siasa Visiwani Zanzibar uliokuwa ukifanyika katika ukumbi wa Salama Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema safari ya kwenda kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyo imara imeshaanza na kasoro zilizogunduliwa na Wataalamu wakati wa utekelezaji zikirekebishwa hatua nyengine ya uimara wa Serikali hiyo itafikiwa vizuri. Alisema Utamaduni uliotumiwa wa kuleta mabadiliko ya Kisiasa Zanzibar bila ya kujali Maslahi ya Mtu au kikundi Fulani bado unahitajika.
“ Utamaduni ule ule wa kustahamiliana na kuvumiliana unahitajika kufikia hatua nyengine tunayoitaka”. Alisisitiza Balozi Seif Ali Iddi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliongeza kwamba imani inaendelea kujengeka kwa wale waliokuwa na mashaka kwa Serikali ya Pamoja iliyopo, hivyo nguvu za pamoja zinahitajika katika kuiunga mkono kwa hali zote.
Alisema ni jambo la kupendeza kuona Wananchi kwa pamoja bila ya kujali itikadi zao za Kisiasa walishirikiana na kufanikisha Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar za Mwaka huu wa 2012 zikiashiria kuwepo kwa Mshikamano baina ya Wananchi wote.
Balozi Seif alitanabahisha kwamba Watendaji walioko Serikalini wako tayari kupokea Changamoto zinazoikabili Serikali ya Umoja wa Kitaifa kutoka kwa washirika mbali mbali.
Alisema Serikali itakuwa makini kuangalia mapendekezo na maazimio yaliyomo katika Mkutano huo kwa lengo la kuifanya kuwa bora na imara zaidi.
“ Serikali itakuwa makini kuangalia mapendekezo hayo ili yaweze kuboresha si Serikali tu bali hata Taasisi nyengine zinazohusiana na Utendaji wa Serikali yenyewe”. Alisisitiza Balozi Seif.
“ Tumesema na tutaendelea kusema na kuhimiza kuwa watendaji wabadilike, wasifanye kazi katika utaratibu wa “ Bussiness as usual ”. Hatutowatendea haki Wananchi na hiyo sio azma ya Serikali hii”. Alifafanua zaidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Alielezea matumaini yake kwamba Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam { REDET } utaendelea kutoa nafasi kwa Zanzibar katika Programu zake ili Jamii ipate kujadili masuala yenye maslahi ya Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
Mapema akisoma maazimio ya washiriki wa mkutano huo Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ambae pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Redet Dr. Benson Bana alisema Mapendekezo ya wadau hao yatafikishwa katika ngazi inayohusika kwa ajili ya hatua za utekelezaji.
Mkutano huo ulijadili mada tano ambazo ni Misingi ya Kikatiba ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Ushirikshwaji wa Wazanzibari na Kujenga Imani ya Wananchi katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Nyengine ni Namna Baraza la Wawakilishi na Serikali { yaani Mihimili ya Utendaji inavyofanya kazi katika Mpangilio wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa pamoja na nini kifanyike kuimarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top