Wazazi wanapaswa kujenga utaratibu wa kufuatilia nyendo za watoto wao kimasomo Maskulini kwa lengo la kukabili vyema Changamoto wanazopambana nazo kila siku.
Kauli hiyo imetolewa na Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi katika hafla ya kukabidhi Vitabu kwa skuli Tano za Sekondari zilizomo ndani ya Jimbo la Dole hapo katika viwanja vya Skuli ya Regeza Mwendo Mwera.
Vitabu hivyo elfu 1046 vimetolewa msaada na Mbunge wa Jimbo la Tarime Tanzania Bara Mh. Nyambani Chacha Mariba anayemiliki Kampuni ya Uchapishaji wa Vitabu ya Nyangwire Buffer Printing Press ya Jijini Dar es salaam vikiwa na thamani ya Shilingi 10,000,000/-.
Msaada huo wa awamu ya kwanza wakati awamu ya pili itakamilishwa mwezi Juni mwaka huu umekwenda sambamba na msaada wa Vifaa vya Maabara kwa Skuli hizo uliotolewa na Bwana Severen wa Kampuni ya Semca kufuatia juhudi wa Mbunge wa Jimbo la Dole Mh. Selveter Mabumba na Mwakilishi wa jimbo hilo Mh. Shawana Bukheit Hassan.Mama Asha alisema kinachohitajika zaidi na Taifa ni Maendeleo. Hivyo juhudi za pamoja zinahitajika katika kufikia lengo hilo.
Aliwataka Wanafunzi waendelee kuwapa moyo Viongozi wao kwa kujitafutia elimu zaidi itakayoamsha ari ya kupatikana kwa misaada ya ziada itakayoondosha changamoto zilizowazunguuka. Katika kuunga mkono jitihada hizo za kusukuma Maendeleo ya Elimu Mama Asha Suleiman Iddi aliahidi kutoa Kompyuta moja na Printer yake ili isaidiae uchapishaji wa mitihani ya majaribio katika Skuli za Jimbo hilo.
Mapema akikabidhi Msaada huo Mbunge wa Tarime Mh. Nyambani Chacha Mariba ameahidi Kampuni yake kuchapisha vitabu vyovyote vitakavyotungwa na walimu vikiwa na Mazingira ya kusomeshea ya Zanzibar.Katika Risala yao Wanafunzi hao wa Skuli tano za Sekondari za Jimbo la Dole iliyosomwa na mwanafunzi Bimkubwa Salum Ali wameahidi kuvitunza Vitabu hivyo.
Wanafunzi hao wameomba kuangalia pia uwezekano wa kupatiwa vikalio ili waondokane na tatizo sugu linalowakabili kwa kipindi kirefu sasa. Skuli hilo Tano za Sekondari za Jimbo la Dole zitakazofaidika na msaada huo wa Vitabu Mchanganyiko wa Masomo mbali mbali ni pamoja na Skuli ya Regeza Mwendo, Dole, Kianga, Langoni na Dole Wazazi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top