Ipo haja kwa Washirika na Wafadhili wa Maendeleo katika nyanja za Elimu ya Dini ndani na nje ya Nchi kufikiria zaidi wazo la kuongeza nguvu katika ujenzi wa Vyuo na Madrasa ili kuwajengea mazingira bora ya Kitaaluma Watoto wa Taifa hili.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya kulifunguwa Jengo Jipya la Madrasa Hidayatul Islamia iliyopo Njia Kuu Moga ndani ya Wadi ya Gamba Wilaya ya Kaskazini A.
Balozi Seif alisema Jamii ya Kiislamu imeshuhudia ongezeko kubwa la Ujenzi wa Misikiti Nchini kasi ambayo inaweza pia kuelekezwa katika Vyuo na Madrasa ambayo Maeneo mengi yamekuwa na ufinyu wa Majengo hao ya Kudumu.
“ Sisemi kwamba Wafadhili wasijenge Misikiti la hasha. Lakini ni vyema kwa wafadhili wakaangalia mazingira ya Vyuo na Madrasa nyingi Nchini ambazo ama ni mbovu au hazina hadhi ya kusomeshea kitabu cha Mwenyezi Muungu ”. Alishauri na Kusisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Mfadhili wa Madrasda hiyo Ukti Asia Mohd wa Oman kwa juhudi zake za kusaidia kupanua Elimu ya Dini Hapa Nchini.
“ Nimevutiwa na Madrasa hii. Nilipoikagua ndani nimeona Darasa la Watu Wazima. Hii ni ishara na fursa nzuri kwa nao kupata wasaa wa kujielimisha. Kwa kweli Madrasa zina umuhimu wa kipekee katika kutanua Elimu popote pale ”. Alifafanua Balozi Seif.
Balozi Seif aliwataka Vijana kuhakikisha wanaitafuta Elimu kwa Njia yoyote huku akiisisitiza Jumuiya inayosimamia masuala ya Elimu ya Dini Wilaya ya Kaskazini “A” { JUVMAWA } ikaendelea kuonyesha Njia bora kwa Watoto wanaowalea.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameahidi kutoa Mchango wa Kompyuta moja kwa ajili ya Madrasa hiyo na kuutaka Uongozi wa Jimbo la Chaani, Wilaya ya Kaskazini A na Mkoa wa Kaskazini kuhakikisha changamoto zinazoikabili Madrasa hiyo zinatatuliwa.
Katika Risala ya Madrasa hiyo iliyosomwa na Ustadhi Khamis Hakim alisema Madrasa hiyo iliyoasisiwa zaidi ya miaka 80 ikiwa na Wanafunzi 500 mchanganyiko imekuwa chemchem ya kutoa walimu wanaoendelea kusomesha Madrasa tofauti Wilayani humo.
Wakati huo huo mamia ya Waumini wa Dini ya Kiislamu na Wananchi wamehudhuria Maulidi ya Uzawa wa Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Mtume Muhammad { SAW }.
Maulidi hayo yaliandaliwa na Uongozi wa Masjid Noor Muhammad { SAW } iliyopo Mtaa wa Mombasa kwa China ambapo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikuwa Mgeni Rasmi kwenye Hafla hiyo.Akitoa chakula cha moyo katika hadhara hiyo Mwanachuoni Maarufu ndani ya Mwambao wa Tanzania Sheikh Sameer Zulfikar amewaasa Waumini wa Dini ya Kiislamu kutouacha Mwezi huu ukapita bila ya kusafisa nyoyo zao kwa kumtukuza Mtume Muhammad { SAW }.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top