Vyama vya Wafanyakazi vinapaswa kupatiwa haki na fursa zote zinazostahiki katika kuruhusiwa kufanya kazi zake kikamilifu bila ya bughudha ya aina yoyote.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohd Sheni alitoa kauli hiyo wakati akifungua Kongamano la kuadhimisha miaka 10 ya Chama cha Walimu Zanzibar liliofanyika katika Ukumbi wa Zamani wa Baraza la Wawakilishi   uliopo Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Akisoma Hotuba  kwa niaba ya Rais wa Zanzibar  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema thamani ya wafanyakazi ni kubwa kwa vile wao ni sehemu ya Serikali.
Alisema Serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na vyama vya Wafanyakazi kutokana na mchango wao mkubwa kwa Taifa hasa wakati wa kupigania Uhuru wa Nchi hii.
Aliwaagiza Watendaji wote wa Serikali kufuata taratibu na sheria zilizomo ndani ya vyama vya Wafanyakazi kwa lengo la kupata fursa zao zinazostahiki.
Aliupongeza  uongozi na Wanachama wa Chama cha Walimu Zanzibar kwa mafanuikio waliyoyapata ndani ya kipindi cha miaka kumi tokea kuanzishwa kwake.
Aliwahakikishia kwamba Serikali itafanya kazi na kuboresha maslahi  ya Walimu kwa kadri ya hali itakavyoruhusu.
“ Ni kweli kuwa hakuna Taifa bora bila ya kuwa na Elimu bora na pia hakuna Elimu bora bila ya kuwa na  Walimu bora. Serikali inalijuwa na tunalizingatia hilo ”. Alifafanua Balozi Seif.
Aliitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali itakapokaa kupitia Muundo wa Walimu ni vyema ikaushirikisha Uongozi wa  Chama cha Walimu Zanzibar ambacho ndio mdomo na masikio ya Walimu.
Akizungumzia kadhia iliyotokea ya Baadhi ya Wanafunzi wa Zanzibar wa Darasa la kumi na mbili kufutiwa Matokea yao Balozi Seif Seif aliwataka Walimu kuwa macho zaidi katika kusimamia vyema Mitihani.
Alielezea kufarajika kwake kusikia ipo Kamati iliyoundwa kuchunguza tatizo hilo ambalo anatajia itatoa matokeo yenye muelekeo mwema kwa Wanafunzi watakaofanya Mitihani yao hapo baadaye.
“ Utamu wa Ualimu unachanua na kupendeza pale anaposikia matokeo mazuri ya Wanafunzi  aliowapa Taaluma ”. Alifafanua Balozi Seif.
Akimkaribisha Balozi Seif Wazizi wa Kazi Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika Mh. Haroun Ali Suleiman alisema katika kuwajenga kimapato Watumishi  Mfuko Maalum utaanzishwa wa uwezeshaji utakaofuata muundo wa mfumo wa Benki ya Kiislamu.
Mapema akisoma Risala Katibu Mkuu wa Chama cha  Walimu Zanzibar { ZATU } Bwana Mussa Omar Tafurwa aliiomba Serikali kuongeza kasi ya Ujenzi wa Nyumba za Walimu hasa Vijijini ili kuondosha tatizo.
Nd. Tafurwa alisema ukosefu wa nyumba za walimu unachangia kuviza maendeleo ya Elimu kwa vile muda wa ufundishaji hupunguwa.
Hafla hiyo ilinogeshwa na Wanafunzi wa Skuli ya Maandalizi ya kidutani kufuatia nyimbo zao safi za asili ambapo Balozi Seif aliahidi kuwazawadia Watoto hao shilingi laki Tatu.
Wakati huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi shilingi laki tano kwa Kikundi cha Utamaduni cha Skuli ya Kiongoni Makunduchi.
Ahadi hiyo aliitowa wakati wa uzinduzi wa Soko la Jumapili tarehe 8 Januari mwaka huu hapo Kisonge ambapo Kikundi hicho kilitumbuiza na kutoa Burdani safi.Fedha hizo aliziwakilisha kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika Bibi Asha Abdulla.
 Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top