Msumbiji imeiomba Tanzania kufikiria uwamuzi wa kurejeshwa tena utaratibu wa kuwa na vikao vya pamoja kati ya pande hizo mbili ambao ulilenga zaidi kuimarisha ujirani mwema.
Ombi hilo limetolewa na Balozi wa Msumbiji Nchini Tanzania Bw. Zakaria Kupella wakati alipofanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Bw. Kupela alisema Tanzania ilikuwa mstari wa mbele katika kusaidia ukombozi wa Mataifa ya Bara la Afrika ikiwemo jirani yake Msumbiji, hivyo ni vyema vikao vya ushirikiano vikafufuliwa kwa nia ya kulinda umoja na udugu wa sehemu hizi mbili.
“ Si jambo la kupendeza kuona sasa ni mwaka wa saba pande hizo hazijakutana katika ule mfumo wa vikao vya ushirikiano. Kikao cha mwisho kilifanyika mwaka 2006 Nchini Msumbiji wakati kile kinachofuata kilitakiwa kifanyika Tanzania ”. Alikumbusha Balozi Kupella.
Balozi wa Msumbiji alisisitiza kwamba yapo maeneo mengi ambayo Wananchi wa pande hizo mbili wamekuwa wakishirikiana pamoja hasa ikizingatiwa kwamba Nchi hizo zimepakana.
Alisema itapendeza iwapo utaandaliwa utaratibu wa kuyaunganisha Makundi ya Vijana wa Pande hizo mbili kujenga Taifa katika mpango wa kujitolea.
“ Ipo miradi ya Jamii kama vile ujenzi wa maskuli na Vituo vya Afya hata visima vya maji ambavyo wanaweza kutumiwa Wanafunzi wa Kujitolea wa sehemu hizo kuongeza nguvu zao ”. Alishauri Balozi Kupella.
Alisisitiza ni vyema kwa nchi hizi zikafaidika pamoja katika kutumia rasilimali zilizomo kwa vile zilishirikiana katika ukombozi.
Balozi wa Msumbiji Nchini Tanzania aliipongeza Zanzibar kwa kumaliza uchaguzi katika njia ya kihistoria iliyopelekea kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa hali ambayo Msumbiji itaendelea kujifunza katika mfumo huo.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alimueleza Balozi wa Msumbiji Nchini Tanzania Bwana Zakaria Kupella kwamba uhusiano wa pande hizo mbili hivi sasa inafaa uelekezwe zaidi katika Uchumi badala ya Siasa.
Balozi Seif aliiomba Msumbiji kufikira wazo la kutoa Wataalamu kuja Zanzibar katika kutoa elimu katika sekta ya Uvuvi wa Kamba.
Alisema Dunia imeshuhudia kiwango kikubwa cha Bidhaa ya Kamba inayozalishwa Msumbiji na kusafirishwa nje ya Nchi na kuipatia kipato kikubwa Nchi hiyo.
Mapama Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana kwa mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya { EU } Nchini Tanzania Bw. Filiberto Ceriani.Katika mazungumzo yao Viongozi hao walielezea haja ya kuongeza ushirikiano kati ya pande hizo mbili.
Bw. Filiberto Ceriani alimueleza Balozi Seif kwamba Umoja wa Ulaya umeandaa mpango wa kuzijengea uwezo Jumuiya na Taasisi za Kiraia utakaogharimu karibu Euro Milioni 3,000,000.
Balozi Filiberto alisema mpango huo utaenda sambamba na utowaji wa mafunzo kwa watendaji wa sekta ya Sheria kwa lengo la kuijengea mazingira Bora ya uwajibikaji Sekta hiyo muhimu kwa Jamii.
Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliuhakikishia Umoja wa Ulaya kwamba Zanzibar inaendelea kupiga hatua za Maendeleo kufuatia uendeshaji wa Mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Hata hivyo Balozi Seif alisema bado yapo maeneo muhimu ya huduma za Kijamii kama maji, Elimu na Afya ambayo hayajafikia kiwango kilicholengwa na msaada zaidi unahitajika kutoka kwa Taasisi na Mashirika hisani ya Maendeleo kuongeza nguvu zao.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top