Serikali itaangalia hali halisi ya namna  gani itakavyotoa maamuzi muwafaka kuhusiana na  Wananchi wanaoishi kwenye eneo lililotengwa  kwa hifadhi ya Misitu liliopo Kiwengwa Pongwe.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameeleza hayo wakati akitoa mkono wa pole kwa Familia nane za Wananchi waliokumbwa na janga la nyumba zao kuteketea  kwa moto hapo Mchekeni Kiwengwa  Wilaya ya Kaskazini ‘‘B’’. 
Ambapo familia Tano za Wananchi hao hivi sasa zimehifadhiwa katika Jengo la Ofisi ya CCM Jimbo la Kitope iliyopo Kinduni na Tatu zilizobaki zimepata hifadhi kwa Majirani wa karibu wa Eneo hilo la Mchekeni.
Balozi Seif alisema ni vyema kwa Serikali  ikatafakari kwa pamoja suala la Makaazi ya Wananchi hao sambamba na  umuhimu wa hifadhi ya Misitu iliyopo katika sehemu hiyo. 
“ Maamuzi yoyote yatakayotolewa na Serikali lazima myakubali. Inawezekana  kuhamishwa au kuendelea  kubakia hapa, lakini cha msingi zaidi ni kutolewa uwamuzi utakaolinda  maslahi zaidi ya jumla ya Taifa ”. Alisisitiza Balozi Seif.
“ Hivi sasa wapo tu kama popo hawana uwezo wa  kujenga makaazi ya kudumu kwa sababu eneo hilo kutangazwa kuwa Hifadhi ya Misitu ”.Balozi Seif  aliendelea kufafanua zaidi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza Wananchi hao kwamba lazima  wawe na uhakika wa Maisha yao yakiambatana pia na shughukli  zao za Kimaisha kama vile Kilimo na harakati za ujasiri amali.
Alisisitiza kwamba  Wanakijiji hivi sasa wanashindwa  na maamuzi ya ujenzi wa nyumba za kudumu kutokana na Mamlaka inayohusika na  misitu kutoruhusu ujenzi katika eneo hilo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiwa pia ni Mbunge wa Jimbo la Kitope alitoa mchango wa Shilingi Laki Nne kuwafariji Wananchi hao kutokana na Janga hilo ili kupata kianzio cha Maisha. Mapema Mjumbe wa Nyumba Kumi { Balozi } katika eneo hilo Nd. Elyas Yaqoub alimueleza Balozi Seif kwamba chanzo cha Moto huo ni Mtoto wa moja ya Familia zilizopata janga hilo kujaribu kusaidia harakati za mapishi kwenye nyumba yao na baadaye kushindwa kudhibiti moto aliokuwa akiuchochea jikoni hapo.
Naye Sheha wa Shehia ya Kiwengwa Bwana Maulid Masoud Ame  alisema Wakaazi wa eneo hilo wanalazimika kuendelea kujenga nyumba za Makuti ambazo ni hatari kwa vile eneo hilo liko katika msongamano wa mawazo.
Bwana Maulid Alisema mbali ya suala hilo lakini hata huduma za maji zimekuwa finyu na kupelekea Wananchi hao kushindwa kukabiliana na Moto huo kutokana na ukosefu wa Maji.
Nyumba nane zilizoungua moto huo zilikuwa zikimilikiwa na Nd. Six Alfred, Kisumo Paulo, Maganga Said, Chales Lukas, Stephano Kabangara, Simon Chales, Tabia Petro na Mwashi Kabangara.Hadi sasa hasara ya gharama ya jumla iliyotokana na kuunguwa kwa Nyumba hizo bado haijajuilikana ambapo baadhi ya Wakaazi hao wamepoteza kila kitu.
 Othman Kahmis Ame 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top