Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameagiza kusitishwa mara moja  kwa shughuli zozote za ujenzi wa Maradi wa Hoteli katika eneo la Nungwi Mashariki lenye ambalo linaukubwa wa Hekta 30.5.
Agizo hilo amelitoa wakati wa ziara yake ya siku tatu ya kutembelea Miradi ya Maendeleo na ile ya Kijamii ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja .
Balosi Seif alisema zipo dalili za ujanja zinazoonekana kufanywa na   Maafisa wachache na kupelekea mgongano na malalamiko ya umiliki wa eneo hilo kufuatia  kufuta kwa mkataba  wa ujenzi wa Mradi wa Kitalii wa Kampuni ya Spice Island kwa madai ya kukiuka masharti.
Balozi Seif alikemea tabia inayofanya na baadhi ya Watendaji wa Idara ya Ardhi ambayo inawabughudhi Wawekezaji na hatimae kuitia aibu Serikali.
“ Inashangaza kuona Idara ya Ardhi inamfutia mkataba muekezaji mmoja kwa kushindwa  kutekelezaa mkataba ndani ya miaka miwili, lakini idara hiyo hiyo kumpa mwekezji mwengine  kwa zaidi ya miaka saba bila ya kumvunjia ”. Balozi Seif alisema lipo jambo katika mradi huo.
“ Kuanzia sasa nasema sitaki kuona shuguli yoyote ya ujenzi inaendeshwa katika eneo hili hadi Serikali Kuu itakapofanya maamuzi baada ya kufanya utafiti wa kina kuhusiana na mgongano huo”. Balozi Seif alikuwa akimuagiza Afisa wa Ardhi Bwana Sanani Baraka kufanya kutekeleza agizo hilo.
Kwa upande waoWananchi wa Kijiji cha Nungwi wameelezea masikitiko yao kutokana na mgongano huo unaopelekea kucheleweshewa maendeleo yao ya Kijamii kupitia makubaliano ya Mradi wa mwanzo ambao tayari ulikuwa umeshakubalika  baina yao na mwekezaji wa awali.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  aliweka jiwe la msingi la Afisi ya Chama cha Ushirika  cha Akiba na Mikopo cha Mkwajuni na kuwapongeza kwa uamuzi wa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2010 ya kuendeleza Vikundi vya Ushirika.
Balozi Seif alisema Wanachama hao bado wanahitaji kukuza Chama chao ili kukijengea mazingira mazuri ya kujipatia mahitaji yao.
Baadaye Balozi Seif aliweka jiwe la msingi la Jengo jipya la Skuli ya Kidagoni iliyoko ndani ya Jimbo La Nungwi.Ujenzi wa Skuli hiyo umekuja kufuatia Watoto wa Vijiji vya Kidagoni na Mwanguo kufuata Elimu katika masafa marefu.
Balozi Seif alisema  nia nzuri ya Wazee wa Vijiji hivyo ni hatua ya msingi ya kuwajengea hatma njema ya Kielimu Watoto wao.Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  amewaomba  Wananchi hao kuwa na subra kutokana na changa moto wanaopambana nazo za bara bara, maji safi na Kituo cha Afya na kusema Serikali inaangalia njia za kuyatatua matatizo hayo.

 Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top