Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha kwamba uhusiano kati yake ya Sudan inaendelea kuimarika wakati wote.Balozi Seif alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Balozi Mpya wa Sudan Nchini Tanzania  Dr. Yassir Mohd Ali aliyefika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Zanzibar na Sudani zimekuwa na uhusiano wa Kihistoria wa muda mrefu hasa katika Sekta ya Elimu.
Alisema Wanafunzi wengi wa Zanzibar wamekuwa wakipata Elimu ya Juu katika vyuo mbali mbali kwenye fani za lugha na Sheria ya Dini ya Kiislamu.
Balozi Seif alisisitiza kwamba Taaluma hiyo inakwenda sambamba na Walimu wa Sudan kutoa Taaluma hapa Zanzibar katika vyuo tofauti hasa katika somo la Dini na Lugha ya Kiarabu.
“ Uwepo wa Chuo Kikuu cha Elimu Chukwani ambacho kiko chini ya udhamini wa Taasisi ya Africa Muslim Agency ya Nchini humo ambacho hivi karibuni nilikuwa mgeni rasmi katika mahfali ya 11 ya chuo hicho ni ushahidi wa uhusiano huo ”. Alisema Balozi Seif.Mapema Balozi Mpya wa Sudan Nchini Tanzania Dr. Yassir Mohd Ali aliahidi kuendeleza uhusiano huo ambao utakuwa chachu ya Umoja Miongoni mwa Mataifa ya Bara la Afrika.
Dr. Yassir alisema Afrika hivi sasa inapaswa kujikita zaidi katika kujiletea Maendeleo na kuachana na migogoro inayoleta migongano miongoni mwa Wananchi wake.
Akigusia mikakati ya kupunguza migogoro ya kisiasa hasa katika  Nchi yake Balozi Yassir alisema Uhuru wa Sudan ya Kusini umepunguza  joto la Kisiasa kati ya pande hizo mbili.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikuwa na mazungomzo ya Ujumbe wa Watu wawili kutoka Kampuni ya Camden Hospitality Group inayojishughulisha na Miradi ya Hoteli za Kimataifa kutoka Nchini Marekani.
Katika mazungumzo yao Kiongozi wa Ujumbe huo Bwana Munir Walji alisema ziara yao imekuja kufuatia mazungumzo yao ya mwaka uliopita kuhusu uwekezaji wa Miradi ya Hoteli za Kimataifa za nyota Tano pamoja na huduma nyengine za Utalii.

 Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top