Katibu Mtendaji wa Mpango wa Nchi za Kiafrika kujitathmini Kiutawala Bora { APRM } Tanzania Bibi Rehema Twalib alisema hayo wakati Ujumbe wa Uongozi wa Bodi ya Mpango huo ulipokuwa ukiwasilisha Ripoti ya Utawala Bora na Mpango Kazi.
Ripoti hiyo wameiwasilisha kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar .
Bibi Rehema alisema dhamira inayopaswa kuchukuliwa hivi sasa ni kuona namna gain uelewa unajengwa kwa Viongozi na Wananchi katika kujuwa mfumo huo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
“ Zipo dalili zinazoonyesha kwamba baadhi ya Viongozi wakiwemo watedaji wa Serikali na hata Wananchi bado hawajaufahamu mfumo huo”. Alisema Bibi Rehema.
Katika suala la Kiuchumi Bibi Rehema alifahamisha kwamba juhudi zinahitajika katika kuhamasisha Sera katika kuharakisha Maendeleo ya Jamii.
Alieleza kuwa Sekta ya Viwanda ambayo hutoa ajira kwa kundi kubwa la Wananchi hasa Vijana bado haijafanya vyema na vizuri likaimarishwa sambamba na uwekezaji Vitega Uchumi.
Akizungumzia suala la Kodi Katibu Mtendaji huyo wa APRM alitahadharia kuachwa kwa tabia inayoendelezwa na baadhi ya Watendaji wa Serikali kuwakatisha Tamaa Wafanyabiashara katika kazi zao.
Bibi Rehema alisema tabia ya watendaji hao kuwatoza kodi mara mbili wafanyabiashara kwenye Biashara zao kati ya Zanzibar na Tanzania Bara ni kuendeleza kero zinazoweza kuepukwa.
Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Nchi nyingi zimekumbwa na migogoro hasa ya Kisiasa na hata ya ardhi kwa sababu ya kushindwa kuweka utaratibu mzuri wa kuiepuka migogoro hiyo.
Balozi Seif alisema Zanzibar imekuwa na uzoefu wa migogoro ya kisiasa kwa muda mrefu tokea miaka ya 50 na hili ndio lililopelekea Wananchi wake kutafuta mbinu za kuondokana na mfumo huo uliodumisha ustawi wa Maisha yao .Hata hivyo alisema kasoro ndogo ndogo bado zipo lakini ikitokea kuchomozwa kwa migogoro ya kisiasa hapa Tanzania ni ya kujitakia wenyewe kwa vile taratibu sahihi za kuendesha Utawala Bora tayari zimeshawekwa.Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif aliipongeza Taasisi hiyo ya Mpango wa Nchi za Kiafrika kujitathmini Kiutawala Bora { APRM } kwa kufanya kazi kubwa ya kuelimisha Jamii za Kiafrika juu ya Utawala Bora.
Ziara ya Ujumbe huo imehusisha pia matayarisho ya ujio wa Uongozi wa Juu wa Taasisi hiyo ya Mpango wa Nchi za Kiafrika kujitathmini Kiutawala Bora {APRM } ambao unatazamiwa kufanya ziara Maalum hapa Zanzibar kuanzia Tareha 2/3/2012 hadi 22/3/2012.
Ukiwa hapa Zanzibar Ujumbe huo utakaoongozwa na Bibi Marista Seruma utakutana na Viongozi wa Juu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Watendaji na hata wawakilishi wa Taasisi na Jumuiya Tofauti.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment