Viongozi wa Taasisi zinazosimamia Miradi ya Jamii Nchini hasa Halmashauri za Wilaya wameshauriwa kupunguza urasimu usio wa lazima katika utekelezaji wa miradi inayopata ufadhili wa Taasisi hisani na Mashirika ya Maendeleo hasa yale ya Kimataifa.
Ushauri huo umetolewa na Uongozi wa Shirika lisilo la kiserikali la Utafiti na Uandishi wa Miradi Nchini Tanzania { RPPWA }
wakati ulipofanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Nyumbani kwake Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Akitoa Taarifa ya Mpango wa kusaidia Halmashauri za Wilaya za Tanzania zikiwemo kumi za Zanzibar Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika hilo la RPPWA upande wa Zanzibar Bw. Ally Omar Al-Barwan alisema miradi mingi inayoanzishwa na Wananchi mara nyingi inakuwa nadra kupata wafadhili hasa wa nje.
Bw. Al-Barwan alisema mfumo wa Shirika lao wa Uandishi tayari umeshakubalika na wahisani na wameweza kutumia fursa iliyopo juu ya ufadhili unaofanywa kupitia hazina kama vile mfuko wa OPEC, BADEA Serikali ya Japan pamoja na Shirika la Misaada ya Maendeleo ya Jamii Nchini Switzerland { Swissfin }.
Alisisitiza kwamba Shirika la Utafiti na Uandishi wa Miradi Tanzania hivi sasa limejikita zaidi katika kuandaa miradi ya Serikali za Mitaa kupitia Halmashauri zake.
“ Tuko katika hatua za matayarisho ya Mradi wa umeme katika Halmahauri ya Wilaya ya Kaskazini “A” na tunachosubiri ni baraka za Serikali ili tuanze kazi mara moja” Alisisitiza Bw. Al-Barwan.
Naye Mkurugenzi Masoko wa Shitika hilo la RPPWA Bw. Anthony Mahuke alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba Sera ya Taifa ya ushirikishwaji Jamii katika Mipango ya Uchumi na Mendeleo umeongezeka vizuri hivi sasa.
Bw. Anthony alisema Jamii imeweza kushiriki katika shughuli za Kiuchumi na Kijamii hatua ambayo imesababisha upanuzi wa ajira miongoni mwa Wananchi hasa kundi kubwa la Vijana.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa RPPWA Bw. Pattric Bettele alifahamisha kwamba Mpango wa Makaazi Mapya { New City Programme } ambao utakuwa ukitekelezwa katika Halmashauri za Wilaya imeshakubaliwa na Wahisani.
“ Huu ni Mapango unaosambazwa na Swissfin Programme kwa Nchi za Afrika. RPPWA tumeona tuuchangamkie mapema kwa vile fursa hii ni nadra kupatikana” Alisisitiza Bw. Pattric Bettele.
Uongozi huo wa Shirkka la Utafiti na Uandishi wa Miradi Tanzania { RPPWA } umemuomba Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kusaidia kuhitimisha taratibu za utiwaji saini Mkataba wa kusimamia Miradi ya Serikali na ile ya Swissfin Programme Corp ili kwenda kwenye Halmashauri zote za Zanzibar.
Akielezea faraja yake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameupongeza Uongozi wa Shirika hilo kwa Juhudi zake za Kizalendo zilizolenga kusaidia Jamii kubwa ya Watanzania.
Balozi Seif aliushauri Uongozi huo kuangalia uwezekano wa kujenga mazingira ya kusaidia sekta ya elimu ambayo imekuwa ikikabiliwa na changa moto kubwa.
Alisema ongezeko la majengo mapya ya skuli yanayohitaji kukamilishwa katika maeneo mbali mbali Nchini limekuwa mzigo mkubwa kwa Serikali hivi sasa.
“ Tumekuwa na changa moto kubwa inayotukabili ya kukamilisha Majengo ya Skuli yaliyojengwa kwa nguvu za Wananchi pamoja na uhaba wa Madeski karibu 35,000 Unguja na Pemba ”. Balozi Seif aliambia ujumbe huo wa RPPWA.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top