Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amefanya ziara fupi ya kukagua Uwanja wa Michezo wa Mao ambao Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko katika mipango ya kutaka kuujenga upya Uwanja huo.
Balozi Seif alikagua Ramani ya eneo la uwanja huo akiwa na Kamati Maalum iliyoundwa ya kuandaa michoro ya uwanja huo.
Miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo ni pamoja na Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohd Aboud Mohd, Waziri wa Habari Abdillahi Jihad Hassan, Waziri Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Fatma Abdull habib Fereji,Waziri wa Mawasiliano na Miundo mbinu Hamad Masoud, Waziri asiye na Wizara Maalum Machano Othman Said na Katibu Mkuu Wizara ya Habari Dr. Saleh Mwinyikai.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema uwamuzi wa Serikali ya kuimarisha Uwanja wa Mao ni kujenga mazingira mazuri ya kusherehekea vizuri zaidi sherehe za Mapinduzi.
Alisema uwanja wa Amani hivi sasa haukidhi mahitaji ya sherehe hizo kutokana na ufinyu wa eneo pamoja na kuepusha hitilafu za uwanja kutokana na gwaride la Vikosi vya Ulinzi ambalo ndio chachu ya sherehe hizo.
“ Kwa kweli bila ya gwaride hakuna sherehe. Na hili ndilo linalowapa nafasi zaidi wananchi kufurahia sherehe hizo” Alisisitiza Balozi Seif.
Wajumbe wa Kamati hiyo walipata fursa ya kujadiliana michoro ya ramani hiyo wakisisitiza kuwepukwa kwa nyumba zilizo karibu na uwanja huo wakati ujenzi utakapowadia.
Uwanja wa Mao ni miongoni mwa Viwanja Vitatu vinavyotegemewa na Wanamichezo kuhudumia michezo kikitanguliwa na kile cha Amani Unguja na Gombani Kisiwani Pemba.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment