Iko haja ya kujiandaa mapema na mipango madhubuti ya muelekeo wa maadhimisho ya kutimia miaka 49 na 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo yanatarajiwa kuwa ya kihistoria kwa kufikia nusu karne.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akiwapongeza Watendaji wa Idara ya Sherehe na Maadhimisho ya Taifa baada ya kufanikisha maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Tarahe 1 Januari mwaka 1964 zilizofikia kilele chake Uwanja wa Amani Mjini Zanzibar hivi karibuni.
Hafla Hiyo fupi iliyoshuhudiwa pia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mh. Mohd Aboud Mohd, Katibu Mkuu Dr Khalid Salum na Naib Wake Nd, Said Shaaban ilifanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi hiyo uliopo Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema sherehe hizo kwa sasa haziko mbali hivyo aliwataka watendaji hao kuendelea kujitolea licha ya kukabiliwa na jukumu kubwa .
“ Nakupongezeni sana kwa kazi kubwa mnayoendelea kuifanya. Hili si jukumu dogo lakini hii yote ni kutekeleza wajibu wenu”. Alisisitiza Balozi Seif.
Balozi Seif aliwanasihi watendaji hao kutovunjika moyo kutokana na hitilafu ndogo ndogo na kusisitiza kwamba malalamiko katika shughuli yoyote ile ni jambo la kawaida.
Akitoa shukrani kwa niaba ya watendaji wa Idara ya Sherehe na Maadhimisho ya Taifa Mkurugenzi wa Idara hiyo NduguIssa Ibrahim Mohd alimueleza Balozi Seif kwamba changa moto walizo pambana nazo ndio njiapekee itakayowasaidia kujipanga upya katika utekelezaji wa majukumu yao.
Naye Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Khalid Salim ambaye ndie katibu wa Kamati ya Sherehe za Maadhimisho ya Mapinuzi ya Zanzibar alisema ipo haja kwa Serikali kuiongeza nguvu Idara hiyo kwa vile inakabiliwa na Jukumu kubwa la Taifa.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment