Makamu wa Pili wa Zanzibar wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema ni wajibu kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu kuendelea kuusifu kwa vitendo wasfu wa Kiongozi  wa Dini hiyo Mtume Muhammad { SAW } ili kufaulu katika matendo yao.
Balozi Seif alisema hayo wakati alipokutana na Uongozi wa Kamati tendaji ya Jumuiya na Milade Nabii inayoratibu Maulidi ya Mfunguo Sita ukiwa chini ya mwenyekiti wake Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji hapo Ofisini kwake vuga  Mjini Zanzibar.
Alisema wajibu huu utafikia lengo iwapo Viongozi wanaohusika na usimamizi huo  watahakikisha wanashirikiana vyema. 
Balozi Seif Aliuomba Uongozi wa Kamati Tendaji hiyo ya Milade Nabii kuonana na Uongozi wa Ofisi yake pale wanapopata matatizo kwa Vile Ofisi hiyo ndio inayoratibu sherehe na maadhimisho yote ya Kitaifa hapa Nchini.
Aliipongeza kamati hiyo kwa juhudi zake zinazopelekea kufanikisha Maulidi ya Mfunguo sita ya kila mwaka.
Mapema Kadhi Mkuu wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo Sheikh Khamis Haji aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ukaribu wake na Taasisi za Kidini hapa Nchini.
Akitoa Historia ya Maulid ya Mfunguo sita yanayofanyika kila mwaka hapa Zanzibar Katibu wa Kamati hiyo Sheikh Shiraly Shamsi alisema Maulid hayo yameanza kusherehekewa hapa Zanzibar tokea mwaka 1926.
Sheikh Shirali alisema kwamba kabla ya hapo Maulidi ya Mfunguo sita yalikuwa huadhimishwa na Waumini kupitia taratibu zao za kifamilia pamoja na Mitaa.
Maulidi ya  mwaka huu yanategemewa kufanyika tarehe 4 febuari mwaka 2012 sawa na mwezi 11 mfunguo sita kutegemea kuandama kwa mwezi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar



0 comments:

 
Top