Asilimia 42.5% ya pato la Zanzibar kwa mwaka 2010 limetokana na Sekta ya Huduma ambayo ndio inayoongoza katika kulipatia pato kubwa Taifa hili.
Akikifungua Kituo cha huduma kwa wateja cha Kampuni ya Simu za mikononi cha Zantel hapo Maeneo huru Amani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema uchumi wa Zanzibar kwa asilimia kubwa un aendelea kutegemea utoaji wa huduma.
Balozi Seif alisema yapo mapungufu mengi katika Sekta hii ambayo ni vyema yakafanyiwa kazi kwa maslahi ya Taifa.
Akatolea mfano wa tabia ya kuwavunjia wateja shughuli zao za kimaisha kwa sababu za kuongojea huduma linafaa kuachwa mara moja.
“ Wateja wengi nikiwemo mimi sipendi kusikia neno “subiri” ambalo kwa sana linaonekana kama neno la kawaida kwa watoa huduma kumbe ni adui mkubwa kwa watoaji huduma hiho”.Alitahadharisha Balozi Seif.
Aliushauri Uongozi wa Kampuni hiyo kusikiliza malalamiko ya wateja kwa lengo la kuepuka mivutano isiyo ya lazma baina ya Kampuni ya Wateja wao.
Balozi Seif pia aliiomba Kampuni hiyo kuendelea kuwajali wateja wao wa Zanzibar ambao ndio waliifundisha tata Zantel na sasa Kampuni hiyo inakimbia kwa haraka.
Katika Salamu za Uongozi wa Kampuni ya Zantel zilizosomwa na Bibi Shinuna Kassim kwa Niaba ya CEO wa Zantel Bwana Ali Hamad Bin Jarsh wamesema uzinduzi huo unakirudisha kituo cha Zantel huduma kwa Wateja nyumbani kwao.
“ Waswahili wanasema Mtu kwao na hii ingekuwa sababu tosha ya kukirudisha kituo hichi nyumbani ”. Alifafanuwa Bibi Shinuna Kassim.
Alisema kamba lengo kuu la kukirudisha kituo hicho Zanzibar ni kuongeza ajira kwa Vijana, Kukuza Kiwahili sanifu kwa wateja wanaotumia Zantel pamoja na kupunguza gharama na kubadilishana faida baina ya mashirika na Makampuni ya Serikali .
Mapema akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Waziri wa Mawasiliano na Miundo Mbinu Mh. Hamad Masoud ameihakikishia Kampuni ya Zantel kwamba Serikali itakuwa pamoja nao katika kuhakikisha huduma bora za Mawasiliano zinawafikia Wananchi.
Mh. Hamad aliishauri Kampuni hiyo ya Zantel kuheshimu Mikataba ya Kazi kwa Wafanyakazi wao ili kuondosha malalamiko yanayojitokeza kwa baadhi ya Wafanyakazi hao.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment