Benki ya Maendeleo ya Kiislamu { IDB } imepongezwa kwa jitihada zake za kusaidia ufadhili kwa Wanafunzi wa Tanzania wanaopata fursa ya masomo ya juu katika Vyuo vikuu vya Mataifa ya Mashariki ya Kati.
Pongezi hizo zimetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya mazungumzo na Ujumbe wa Benki hiyo ukiongozwa na Meneja wake Bwana Malik Shah hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema Hatua ya Benki hiyo inafaa kuungwa mkono na Taasisi nyengine katika dhana ya kuona kizazi cha sasa kinapata taaluma ya kina kulingana na mabadilio ya Sayansi na Teknolojia Duniani.
“ Nimeshuhudia harakati za Wanafunzi wa Kitanzania katika miaka ya 80 wakipatiwa viza Mjini Nairobi kupitia ufadhili wa Benki hiyo, wakati huo mimi nikifanya kazi katika Taasisi ya Mambo ya nje ya Tanzania ”. Alifafanua Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuelezea ujumbe wa Benki ya Maendeleo ya Kiislam kwamba licha ya Tanzania ikiwemo Zanzibar kwa jumla kuendelea kuongeza vyuo vikuu lakini bado wimbi la wanafuzi wanao sifa za kujiunga na vyuo hivyo ni kubwa.
Balozi Seif aliushauri Uongozi huo kuendelea kuongeza fursa zaidi wakilenga pia Fani ya sayansi ambayo inaonekana kukosa Wataalamu.
“ Tunahitaji nafasi za masomo zaidi katika fani ya sayansi kwa vile bado Taifa linaendelea kuhitaji Wataalamu wa fani hiyo ”. Alisisitiza Balozi Seif.
Naye Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kiislamu Bwana Malik Shah ameahidi Taasisi yake kuendelea kusaidia ufadhili wa Masomo ya juu kwa Wanafunzi wa Zanzibar.
Bwana Malik alimueleza Balozi Seif kwamba sulala la Wanafunzi wa Zanzibar ataliwasilisha kwenye uongozi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi hiyo kwa kuchukuliwa hatua zaidi.
Benki ya Mendeleo ya Kiislamu { IDB } imekuwa ikitoa ufadhili kwa Wanafunzi wa Kitanzania kupata elimu ya juu katika Mataifa ya Malaysia, Turky na Jordan.

0 comments:

 
Top