Kasi ya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto inayoonekana kuendelea kushamiri nchini inatishia amani ndani ya jamii na hapana budi kupigwa vita na makundi ya rika zote.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto yaliyofanyika huko Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Balozi Seif alisema Takwimu za udhalilishaji dhidi ya Wanawake zinaonyesha kuwepo kwa ongezeko kubwa la vitendo vya ukatili kwa Wanawake mwaka huu wa 2011 ikilinganishwa na mwaka 2010.
Alisisitiza kwamba Serikali katika jitihada zake za kupambana na vitendo hivyo itahakikisha Sheria zinazowalinda wanawake na Watoto zinakwenda na wakati na kutoa fursa ya haki kutendeka.
“ Naamini siku ambayo sisi wanaume tutaamua kuachana na vitendo hivi vya ukatili dhidi ya wanawake itakuwa ndio mwisho wa maadhmisho hayo hapa kwetu. Kwa nini tuadhimishe kitu ambacho hakipo ? ”. Alihoji Balozi Seif.
“ Suala langu kwa wanaume wenzangu tuliohudhuria hapa na wanaotusikiliza, lini tutaamua kuachana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ? ”. Balozi Seif aliendelea kuhoji kutokana na kukera na jambo hili.
Alitahadharisha kwamba wanaoendesha vitendo hivi vya ukatili wa Kijinsia waelewe kwamba vitendo vyao hivyo viovu ni sawa na kutangaza vita dhidi ya Taifa.
Balozi Seif alisisitiza kamba Maazimio na Matamko mbali mbali ya Kitaifa na Kimataifa yamekuwa yakitolewa na kuridhiwa na nchi mbali mbali Duniani ikiwemo Tanazania ya kukomesha aina zote za unyanyasaji na ukandamizaji wa Wanawake na Watoto.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ameliagiza Jeshi la Polisi kuandaa utaratibu maalum kwa watu wanaohusika na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia hasa ubakaji ili kudhibiti kuongezeka kwa vitendo hivyo.
Alisema utaratibu huo ulenge kuwaondolea dhamana wabakaji hao na kuwaagiza Polisi na Mahakama kuacha kutoa dhamana kwa wakorofi hao.
Akitoa Taarifa Mratibu wa Polisi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake Mkoa wa Kaskazini Unguja Kamanda Hasina Ramadhan Taufiq amesema matendo ya udhalilishaji wa kijinsia ndani ya mkoa huo yamepanda kutoka 52 mwaka 2010 hadi 103 mwaka huu.
Kamanda Hasina alisema hali hii inazidi kila kukicha kutokana na kukosekana kwa mapungufu mengi likiwemo lile la utolewaji wa ushahidi mahakamani na kupelekea kutolewa hukumu kwa watuhumiwa wawili tu mwaka uliopita na mtuhumiwa mmoja mwaka huu.
Naye Mratibu wa shirika la Misaada ya Maendeleo la Action Aid Bibi Khadija Ali Juma akitoa salamu za shirika hilo ambalo ni mshirika mkuu wa kundi la wanawake amesema Taasisi yakeitaendelea kusaidia wanawake kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujiamini katika mazimngira wanayoishi.
Bibi Khadija alisema Action Aid imeongeza nguvu zake zaidi za huduma Kaskazini unguja kwa vile nimkoa uliokumbwa na matendo ya udhalilishaji wa kijinsia kwa Wanawake na Watoto.
Katika risala yao wana jumuiya ya Wanawake Mkoa Kaskazini Unguja iliyosomwa na Katibu wake Bibi Siti Ali Makamae wamesema udhallishaji Mkoani humo unaongezeka kutokana na ucheleweshaji wa hukumu kwa watuhumiwa.
Walisema amani, Ulinzi na Usalama unakosekana ndani ya jamii kutokana na kushamiri kwa vitendo hivyo vinavyopelekea kuathirika kiakili kwa wanaodhalilishwa kijinsia.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top