Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kukipatia vifaa na Mitambo ya kisasa kiwanda cha Idara ya upigaji chapa cha Serikali ili kitekeleze vyema majuku yake katika mazingira ya sasa ya Sayansi na Teknolojia.
Kusudio hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipofanya ziara fupi ya kuangalia shughuli za kiwanda hicho kiliopo Mkele Saateni mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema Serikali na Jamii imeshuhudia kazi kubwa inayofanywa na wafanyakazi wa Kiwanda hicho, Hivyo ni vyema Serikali ikahakikisha kwamba mazingira ya watendaji hao pamoja na Vifaa vya kisasa vinawekwa na kuimarishwa.
Amewapongeza Wafanyakazi wa Idara hiyo kwa utekelezaji wa majukumu yao licha ya uchakavu wa Vifaa na mazingira magumu ya kazi.
Aliwataka kuendelea kuwa wabunifu zaidi kwa lengo la kuongeza mtaji wa Taasisi yao pamoja na mapato ya Serikali.
“ Si kazi rahisi inayofanywa hapa kwa vile tumeshuhudia wenyewe kumbu kumbu za majukumu mnayoyatekeleza kila siku ikiwemo Uchapaji wa vitabu vya bajeti na miswaada ya serikali ”. Alisema Balozi Seif.
Aliwahakikishia wafanyakazi hao kwamba kadhia inayowakabili ya kujaa kwa maji katika eneo lao la kiwanda na kusitisha kazi zao itaondoa kufuatia Serikali kujiandaa kukihamisha kiwanda hicho na kukipeleka Maruhubi katika majengo ya ilichokuwa Kiwanda cha Sigara.
Wakielezea matatizo yao Baadhi ya Wafanyakazi hao wamelalamikia ukosefu wa upatikanaji wa fedha wakati wanapokwenda likizoni.
Wamesema tatizo hilo limekuwa sugu na kupelekea kuwakatisha tamaa jambo ambalo linawapunguzia ari ya kazi pamoja na ugumu wa maisha wakati wawapo likizoni.
Akitoa Taarifa fupi ya utekelezaji wa kazi wa Idara ya Upigaji chapa Mkurugenzi wa Idara hiyo Nd. Iddi Suwedi amesema utekelezaji wa majukumu yao umekuwa ukisuasua kutokana na Uchakavu wa Vifaa na Mitambo ya kufanyia Kazi.
Nd. Suwedi amesema katika Malengo ya kuiongezea nguvu Idara hiyo mipango inaandaliwa kurejesha tena Bohari kuu kuwa katika mamlaka ya Idara hiyo ili kupata ufanisi na kutoa huduma bora kwa wateja wao.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifika Shirika la Utalii Liliopo katika Jengo la Kihistoria la Livingston liliopo Kinazini Mjini Zanzibar.
Balozi Seif aliagiza jengo hilo likaendelea kupewa hadhi yake iliyokusudiwa ya kuwa sehemu ya Kihistoria na kuacha kutumiwa kama Afisi za kawaida.
“ Tumekuwa watu wa ajabu kweli sijui kwa nini hatuna tabia na utamaduni wa kupenda kutunza Historia yetu “ Alihoji Balozi Seif.
Naye Meneja wa Shirika la Utalii Zanzibar Bibi Sabah Saleh alisema kwamba Jengo hilo maarufu la Livingston tayari limeshafanywa kuwa kielelezo cha Historia hapa Zanzibar.
Othman khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top