India inakusudia kuongeza nafasi za masomo ya elimu ya juu kwa Wanafunzi wa Tanzania katika kipindi kijacho cha mwaka 2012 katika fani ya kilimo na Ufundi.
Balozi wa India Nchini Tanzania anayemaliza muda wake Bw. Bhagirath ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi hapo Afisini kwake Vuga Mjini Zanzibar .
Bw. Bhagirath alisema ongezeko hilo la fursa za masomo litakwenda sambamba na mpango wa utoaji wa mafunzo ya amali ambao uko katika hatua za matayarisho.
Alisema ushirikiano mwema uliopo kati ya India na Tanzania ikiwemo Zanzibar kwa ujumla umewezesha kunyanyua kiwango cha Taaluma kwa Vijawa waliowengi Nchini Tanzania.
Balozi Bhagirath alifahamisha kwamba katika uendelezaji wa uhusiano huo India imeamua kugharamia mafunzo ya Teknolojia ya Habari {Teknohama } yatakayofanyika hapa Tanzania.
“ Walimu wa Mafunzo hayo yatakayochukuwa takriban wanafunzi 100 wa Tanzania Bara na Zanzibar wanatoka India wakati mfuko wa gharama tayari umeshatengwa ”. Alisisitiza Balozi Bhagirath.
Balozi wa India Nchini Tanzania amepongeza kutokana na ushirikiano wa karibu aliyoupata wakati alipokuwa akitekeleza majukumu yake aliyopangiwa hapa Nchini.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameelezea kuridhika na Utumishi wa Balozi Bhagirath uliopelekea kusaidia vyema Maendeleo ya Tanzania.
Balozi Seif alisema Mpango wa India wa kufikiria kuanzisha Mafunzo ya Amali unaweza kuwa mkombozi kwa Vijana wengi wanaomaliza masomo yao hasa ya Darasa la 12 { Form 1V }.
“ Tumekuwa na kundi kubwa la Vijana wanaomaliza masomo yao ya Form 1V likiwa halina muelekeo. Sasa Mafunzo hayo yatapunguza wimbi la Vijana hao kuzurura mitaani bure ”. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alimshauri Balozi Bhagirath kuangalia Nchi yake uwezekano wa kutoa mafunzo kwa wakulima kuhusu matumizi ya mazuri ya maji ambayo Zanzibar imebarikiwa kuwa na rasilmali hiyo muhimu.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top