Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haipendelei kuona masuala ya Kidini yanaingizwa ndani ya fani na Michezo .
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi ametoa kauli hiyo hapo Katika Ofisi ya CCM Jimbo la Kitope iliyopo Kinduni wakati akikabidhi Seti za Jezi za Mchezo wa Soka na Mipira kwa Timu 23 zilizomo ndani ya Jimbo la Kitope.
Balozi Seif alisema mbinu zinzotumiwa na baadhi ya watu kwa visingizio vya dini katika kuzuia Vijana kuendesha miradi yao hasa wakati wa siku kuu zimekuwa zikileta mgongano kati ya pande hizo katika maeneo mbali mbali Nchini.
Aliwataka Vijana kuendelea kukodisha Viwanja vyao kwa kujipatia fedha za kujikimu mahitaji yao huku akiutaka uongozi wa Wilaya na Masheha wanaohusika katika maeneo hayo kuandaa utaratibu wa matumizi ya Viwanja hivyo.
“ Lazima Vijana watumie Viwanja vyao kwa maslahi ya Timu zao kwa vile kila mwaka hukabiliwa na matatizo ya fedha za usajili ”. Alisema Balozi Seif.
Aliipongeza Timu ya Soka ya African Boys ya Jimbo hilo ambayo imefanya vyema katika mashindano mbali mbali na kutambuliwa katika maeneo mbali mbali ya Kisiwa cha Unguja.
Tunataka Timu nzuri itoke Kitope, na hii itawezekana iwapo vijana wanapenda kufanya mazoezi ambayo ndio ushindi katika Michezo ”.
Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi Seti za Jezi na Mipira 46 kwa Timu za Soka 23 zilizomo ndani ya Jimbo la Kitope.
Aliahidi kuendeleza utaratibu wake wa kila mwaka wa kuvipatia nyenzo vilabu vyote vilivyomo ndani ya jimbo lake ili kuhakikisha wanaliletea sifa Jimbo hilo katika mashindano ya kanda,Wilaya na Taifa kwa jumla.
Vifaa Hivyo vya Michezo vimegharimu Jumla ya Shilingi za Kitanzania milioni 2,990,000/- .
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment