Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajia kupokea Ripoti Maalum siku chache zijazo kutoka kwa Tume iliyoundwa kuchunguzwa chanzo cha kuzama kwa Meli ya M.V Spice Islanders katika Mkondo wa Nungwi Mkoa Kaskazini Unguja usiku wa kuamkia Tarehe 10 Septemba mwaka 2011.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa kauli hiyo hapo Afisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mh. Elaston Mbwilo aliyefika kukabidhi mchango uliotolewa na Wananchi wa Mkoa huo kusaidia Kamati ya Maafa Zanzibar kufuatia msiba wa ajali ya M.V Spise Islanders na kusababisha Vifo vya Watu 206.
Alisema Ripoti hiyo ndio itakayokuwa sahihi ya tukio zima lililopelekea jamii kupata mtafaruku uliosababishwa na kauli Tofauti za baadhi ya Watu zilizosababisha kuwachanganya Wananchi.
Balozi Seif lisema Licha ya kazi kubwa inayowakabili wajumbe wa Tume hiyo kufanya Uchunguzi lakini kazi inakwenda vyema na Serikali imewahakikishia Wananchi kwamba Ripoti hiyo itafanyiwa kazi na uadilifu utatumika katika kuona haki inatendeka kwa kila muhusika wa tukio hilo.
Amewatoa hofu Wananchi kwamba Fedha zinazoendelea kutolewa na Wahisani mbali mbali kuchangia mfuko wa Maafa hazijaguswa kabisa kwa matumizi mengine yaliyo nje ya utaratibu.
‘‘ Hatujagusa hata Senti moja katika Fedha zilizotolewa na Wahisani na Watu mbali mbali kuchangia Mfuko wa Maafa. Hata Gharama za Tume iliyoundwa kuchunguza chanzo cha Ajali ya Meli ya M.V Spice zimetolewa kutoka Mfuko wa Serikali ’’. Alifafanua Balozi Seif Ali Iddi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alifahamisha kwamba Hivi sasa Ofisi yake iko katika matayarisho ya kuandaa Ripoti kuhusu makusanyo ya fedha za Michango ziliyotolewa na wahisani ili ipelekwe Serikalini kupata maamuzi ya namna zitakavyotumika fedha hizo.
Lakini Alisisitiza kwamba lengo litakuwa lile lile la kuwagusa moja kwa moja wahusika wa Tukio hilo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Aliwapongeza Wananchi wa Mkoa wa Manyara kwa moyo wao wa kuguswa na tukio hili lililowapata wananchi wa Zanzibar.
Mapema Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mh. Elaston Mbwilo alisema wao kama Watanzania wengine walikuwa na haki ya kuguswa na msiba huo ambao ni wa Kihistoria kuwahi kutokea Zanzibar.
Mh. Mbwilo Aliwataka wananchi kuendelea kuwa na subra wakati wanapopatwa na Majanga mbali mbali ambayo baadaye pelekea kuleta maafa.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment