MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR BALOZI SEIF ALI IDDI AKIWAHUTUBIA WAHITIMU WA MAHAFALI YA TANO YA CHUO KIKUU CHA ARUSHA, KATIKA HOTUBA YAKE BALOZI SEIF ALIZITAKA TAASISI ZA ELIMU NCHINI KUHAKIKISHA KUWA IDADI YA WANAFUNZI WA KIKE KUINGIA VYUO VIKUU INAONGEZEKA ILI KUKIDHI MAHITAJI YA JAMII
Taasisi za Elimu ya Juu Nchini zina wajibu wa kuhakikisha idadi ya wanafunzi wa Kike kuingia Vyuo Vikuu inaongezeka ili kukidhi mahitaji ya Jamii.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameeleza hayo kwenye mahafali ya tano ya Chuo Kikuu cha Arusha ambapo jumla ya wahitimu 600 wamemaliza masomo yao ya shahada ya kwanza na Diploma katika Fani za Biashara, elimu na Ustawi wa Jamii.
Balozi Seif alisema ongezeko hilo litaondosha kabisa pengo kubwa liliopo kati ya Wanafunzi wa Kike na Kiume katika Elimu ya Vyuo Vikuu hapa Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuagiza Uongozi wa Chuo Kikuu cha Arusha kuongeza Mikakati madhubuti ili kuleta uwiano wa Wananfunzi wa Jinsia zote.
“ Tafiti zinaonyesha kwamba kumuelimisha Mwanamke sawa na kuwaelimisha watu kumi. Hii inamana kwamba familia itaelimika haraka iwapo kutakuwa na mmoja wa Mwanamke aliyepata elimu” Alisisitiza Balozi Seif Ali Iddi.
Alifahamisha kwamba vyuo Vikuu Vikuu lazima vishirikiane na Serikali katika kuona Dira ya Taifa ya Maendeleo ishirini ishiri { Vission 2020 } inafikia malengo yake.
Balozi Seif aliitaja changamoto inayowakabili wana vyuo Vikuu ni namna gain wanaweza kutumia Taaluma yao kushajiisha Sekta Binafsi katika kuibua ajira ndani ya Jamii.
Alisema hatua hiyo itakwenda sambamba na mipango ya Serikali zote mbili za kuandaa mazingira bora ya kuongeza fursa katika soko la ajira hasa kwa kundi kubwa la Vijana.
Katika risala yao iliyotolewa na Rais wa Serikali ya Wanafunzi Chuoni hapo Nd. Joshua Onyango wameiomba Serikali kuwapunguzia matatizo yanayowakabili ya Ubovu wa Bara bara, Huduma za Maji safi pamoja na Huduma za Umeme.
Wamesema matatizo hayo kwa kiasi kikubwa yanachangia kupunguza ari yao ya kujipatia Taaluma kwa utulivu ambayo ndio lengo la kuwepo kwao Chuoni hapo.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Arusha Dr. Laban Mgedi alisema lengo la chuo hicho ni kuongeza asilimia 32% ya wanafunzi wa kike Chuoni hapo.
Dr. Laban amefahamisha kwamba Afrika inahitaji wasomo wa fani tofauti wakiwemo wanawake ili kuleta Mapinduzi ya haraka ya Elimu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika Mahfali hayo pia aliweka jiwe la Msingi la Jengo la Michezo la Chuo hicho.
Jengo hilo linalotarajiwa kukamilika ujenzi wake mwezi Febuari mwakani linatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi za Kitanzania Milioni mia mbili.
Kukamilika kwa jengo hilo kutatoa afuaeni kwa wanafunzi kuwa na darasa la uhakika la masuala ya Sanaa na Utamaduni chuoni hapo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment