Indonesia imeahidi kulifanyia kazi mara moja ombi la Zanzibar la mpango wake wa kuimarisha huduma za usafiri wa kudumu wa meli kubwa za abiria na mizigo kati ya Visiwa vya Unguja na Pemba.
Ahadi hiyo imetolewa na Ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Indonesia Unaoongozwa na Waziri wa Nchi anayesimamia Wizara za Biashara na Viwanda na ile ya Maendeleo ya Taifa ya Nchi hiyo Bw. Lee Shyan wakati ulipokutana kwa mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.
Ujumbe huo umesema juhudi za haraka zitaanzishwa kwa kuwasiliana na Makampuni ya Meli Huko Japan ili kuona utekelezaji ya ombi hilo unafanikiwa katika kipindi kifupi kijacho.
Waziri wa Nchi anayesimamia Wizara ya Biashara ya Indonesia Bw. Lee Shyan alimueleza Balozi Seif kwamba Ujumbe wake umekuja Zanzibar kuangalia maeneo ambayo wanaweza wakashirikiana na Zanzibar katika kuwekeza Vitega Uchumi.
“ Naimani kwamba yapo maeneo mengi hasa katika sekta za Biashara, Kilimo na Mtandao wa Mawasiliano ambayo tunaweza kuwekeza au kuingia katika ubia ”. Alisema Bwana Lee Shyan.
Bwana Lee alifahamisha kwamba miradi ya pamoja kati ya pande hizo mbili inaweza kusaidia kuongeza kasi ya maendeleo na kustawisha jamii za sehemu hizo.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliuambia Ujumbe huo kwamba Zanzibar hivi sasa iko katika Mipango ya kukabiliana na Tatizo la Usafiri wa Baharini Kati ya Unguja na Pemba.
Balozi Seif alisema Uanzishwaji wa mradi wa usafiri kati ya Visiwa Hivi mbali ya kutoa ajira pia utatoa kiwango kikubwa cha mapato kwa vile jamii ya Visiwa hivi inategemea sana meli kulingana na mazingira yao ya kimaisha.
“ Wananchi wengi hasa wafanyabiashara ndogo ndogo wa Zanzibar hutegemea zaidi usafifi wa Meli katika kuendesha Biashara zao zinazozunguuka ndani ya mwambao wa Afrika Mashariki ”. Alifafanua Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishauri Indonesia kuingia katika soko la Zanzibar kwenye maeneo ya viwanda vya samaki, Utalii na hata kwa kubadilishana Utaalamu katika masuala ya Biashara ili kustawisha kizazi cha sasa.
Alisema Zanzibar imekuwa na mawasiliano ya Kibiashara ya muda mrefu kati yake na Mataifa mengi ya Bara la Asia.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top