TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohd Sheni amesema suala la usalama wa chakula kitaifa na kimataifa linahitaji kuangaliwa na kushughulikiwa ipasavyo ili kuhakikisha upungufu wa Chakula hautokei.
Dr. Sheni ametoa kauli hiyo wakati akiufungua mkutano wa sita wa Baraza la Biashara la Zanzibar huko katika ukumbi wa Mikutano wa Salama Bwawani Mjini Zanzibar.
Rais wa Zanzibar Dr.Ali Mohd. Sheni akiwa pia Mwenyekiti wa Baraza hilo amesema utaratibu mzuri wa kuzalisha, kuagiza na kuhifadhi chakula unahitajika ili Taifa lijiweke katika hali ya usalama.
Amesema mabadiliko ya matumizi ya chakula yanayotokea Duniani hivi sasa hasa yale ya vyakula vya nafaka yameongezeka kwa kiasi kikubwa sana.
Ametahadharisha kwamba uhaba wa chakula unapojitokeza popote pale huchangia njaa, maradhi pamoja na kusababisha kuyumba kwa uchumi na utulivu wan nchi.
Ameshauri sehemu zote zinazohusika na utoaji wa tahadhari juu ya usalama wa chakula ni vyema zikafanyiwa mapitio na kufanyiwa marekebisho ili zifanye kazi kwa ufanisi ndani ya kitengo cha usalama wa chakula.
Mapema waziri wa Biashara Viwanda na Masoko Mh. Nassor Ahmed Mazui amesema ukuaji wa maendeleo ya Zanzibar utakuwa ndoto kama hakukuwa na ushirikiano kati ya sekta za umma na zile Binafsi.
Mh. Mazrui amesema sekta Binafsi inaweza kufanya maajabu endapo itajengewa mazingira Bora ya Kimiundombinu.
Akitoa Taarifa ya Baraza la Taifa la Biashara Tanzania Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Phelomon Luhanjo amesema utafiti wa muda mrefu umethibitisha kwamba Zanzibar bado ina eneo zuri la kuendeleza Sekta ya Biashara .
Wakichangia katika mkutano huo baadhi ya Washiriki wameeleza kwamba Wananchi na baadhi ya wafanyabiashara wazalendo wameshindwa kutumia fursa zilizotolewa na ZIPA badala yake wameziuza kwa wageni na hatimae kuleta lawama zisizo na msingi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top