Taarifa kwa waandishi wa Habari
Taasisi ya Swahili Performing Arts Center, kwa kushikiana na Ubalozi wa Norway nchini Tanzania na kwa hisani ya kampuni ya mawasiliano ya Zantel inapenda kutoa taarifa ifuatayo kwa vyombo vya Habari juu ya kuendelea kwa mradi wa 100% Zanzibari: shangwe za maridhiano na umoja wa kitaifa Zanzibar.
Mradi wa 100% Zanzibari (Mzanzibari asili mia moja): shangwe za maridhiano na umoja wa kitaifa, wiki hii umeendelea katika mjini Mkoani, Mkoa kusini Pemba.
Katika awamu hii, kikundi cha Tinge kutoka kijiji cha Tundauwa kinawakaribisha wacheza Msewe wa asili kutoka kijiji cha Kambini-Kichokochwe, Mkoa Kasakazini Pemba.Kama ilivyo ada ya mradi huu, wasanii wa kutoka vikundi hivyo viwili watafunga kambi ya siku 5 ambayo tayari imeanza tangu tarehe 11 Oktoba na ambayo itafungwa kwa kupitia onesho la wazi kwa wakaazi na wageni wa Mkoani.
Onesho hilo, linalotegemea kuvutia wengi mjini hapo, limepangwa ufanyika katika uwanja wa Umoja ni Nguvu kuanzia saa 4.30 alasiri.
‘Tumejitayarisha vilivyo kwa kuhakikisha kuwa tunaishajihisha hadhira katika kusherehea maridhiano yetu ambayo yametupa matumaini ya umoja na hatimaye maendeleo katika nchi yetu,’alisema msanii Naomba Othman kutoka kikundi cha Msewe wa Kambini.
Onesho hilo katika mji wa Mkoani linafuatia lile la ufunguzi wa mradi huo uliofanyika katika ukumbi wa Ngome Kongwe-Unguja ambapo miamba ya Taarab, Nadi Ikhwan Safaa na Culture Music Club, ilirindima usiku wa tarehe 8 0ktoba kutokana na burdani mwanana ya muziki wa Taarab iliyopigwa maalum kuzindua mradi wa 100% Zanzibari.
Wananchi na wageni mbali mbali walijimwaga katika ukumbi wa Mambo Club uliomo ndani ya viwanja hivyo, walivipokea vyema vikundi hivyo ambavyo vilipanda jukwaani kukata utepe wa Mradi huo wa miezi miwili (4 oktoba hadi 3 Disemba) utakao ambatana na muziki wa Taarab, Ngoma na Maigizo.Mradi wa 100% Zanzibari umeandaliwa na Kituo cha Sanaa za Maonesho asilia cha Waswahili cha hapa Zanzibar, chini ya ufadhili wa Ubalozi wa Norway nchini Tanzania na kampuni ya mawasiliano ya Zantel.
Katika usiku wa ufunguzi vikundi vya Culture na Nadi Ikhwan Safaa vilipanda jukwaani kwazamu na hatimaye kwa pamoja katika kuonyesha umoja wa wasanii wa vilabu hivyo kupitia mradi huu. Nyimbo zilizotumbuiza usiku huo ni pamoja na ‘Mpunga’ iliyoimbwa na Fatma Dawa, ‘Kama Nilivyonipa’ (Sabrina Hassan), ‘Bahati’ (Amina Juma), ‘Nisubiri hadi lini’ (Mtumwa Mbarouk), ‘Tunapendana’ (Mgeni Khamis),kabla mkongwe Makame Faki hajahitisha kwa wimbo iliowakuna wengi, ‘Vya kale dhahabu’. Nyengine zilikuwa ni ‘Hata Haikuwa’ (Baadie Omar), ‘Ua’ (Raifa Mosi), ‘Kwangu Amepoa’ (Sameer Basalama), ‘Nampenda Mpenzi Wangu’ (Fauzia Abdalla), ‘Leo tena’ (Saada Mohamed), ‘Nchi Yetu’ (Fauzia Abdalla na Mgeni Khamis), ‘Sabal-kheir Mpenzi’ (Kesi Juma na Mtumwa Mbarouk) na mwisho kumalizia na ‘Cheo Chako’ (Fauzia Abdalla).Akizundua mradi huo, Waziri wa Habari, Utamadauni, Utalii na Michezo Mheshimiwa Abdilahi JihadHassan, alipongeza hatua ya kituo hicho kubuni tamasha hilo na kuzishauri taasisi nyengine kuiga mfano huo kutokana na umuhimu wa kujenga maelewano kati ya wananchi wa Zanzibar.
Kufuatia kambi na onesho la Mkoani , kisiwani Pemba, tamasha hilo litahamia Mkoa wa Kusini Unguja kuanzia tarehe 18 hadi 22 Oktoba. Vikundi vitakavyoshiriki katika kambi hiyo na onesho lake katika kijiji cha Makunduchi ni Mpe Chungu (Unguja) na Profesa Gogo na kundi lake na Maendeleo (Kangagani, Pemba).
Kheiri A.Y. Jumbe
Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji

0 comments:

 
Top