Wahitimu wa Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya Zanzibar wamehimizwa kuwa tayari kufanya kazi popote watakapopangiwa ambapo watakuwa na wajibu wa kuthamini na kuchangia jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kupambana na maradhi mbali mbali yanayoisumbua jamii Nchini.

Himizo hilo limetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein kwenye Mahafali ya 22 ya Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya Zanzibar yaliyofanyika kwenye Kampas ya chuo hicho yaliyopo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Jumla ya wahitimu 440 wa kada saba walihitimu na kufanikiwa kupata stashahada mwaka huu wa masomo kukiwa na ongezeko kubwa mara mbili ikilinganishwa na wahitimu 280 wa mwaka 2014.

Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein ambae Hotuba yake ilisomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idii alisema wapo baadhi ya baadhi ya wahitimu wanaoajiriwa na Wizara ya Afya wanapiga chenga kufanya kazi Kisiwani Pemba wakisahau kwamba Wananchi wa kisiwa hicho wanahitaji kupata huduma zao.

Alisema watumishi wa Umma wakiwemo wa sekta ya afya wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na taratibu za kazi na miongozo ya sehemu wanazoajiriwa na inapendeza zaidi wawe mfano wa tabia njema kwa kushikamana katika kutekeleza maadili ya kazi zao.

“ Nimefurahi kusikia kuwa katika orodha ya wahitimu wetu wa fani za afya chuoni hapa wapo waliotoka Tumbatu, Kojani, Fundo, Mtende, na Maeneo mengine ambayo watu wengi huwa wanaona tabu kwenda kufanya kazi kutokana na mazingira ya Kijiografia yaliyopo “. Alisema Dr. Shein.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliiagiza Wizara ya Afya kufanya tathmini ya mahitaji ya wataalamu wa afya katika maeneo hayo ili kujua changamoto zilizopo na hatua za haraka zichukuliwe zitakazowezesha vijana kutoka maeneo hayo wanaajiriwa.

Alisisitiza kwamba Wizara ya Afya ihakikishe inaweka utaratibu kwa lengo la kuwawezesha Vijana wanaopangiwa katika maeneo hayo wanafanya kazi kwa kipindi ambacho Wizara itaona kinafaa bila ya kukiuka sheria za mikataba ya kazi.

Akizungumzia suala la uwekezaji katika sekta ya Afya Nchini Rais wa Zanzibar alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikishajiisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza katika sekta hiyo muhimu jambo ambalo limekuwa likisaidia sana katika kuimarisha huduma za afya Nchini.

Alisema juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha huduma za afya kwa kushirikiana na wawekezaji na washirika wa maendeleo zimekuwa na mchango mkubwa katika kukuza pia soko la ajira hasa kwa wahitimu wa Chuo hicho.

“ Mwezi Machi mwaka huu nilialikwa kuifungua Hospitali ya Tasakhtaa inayoendeshwa na Global Hospitals ya India katika Mtaa wa Vuga. Hii ni Hospitali ya kisasa yenye uwezo mkubwa wa kutibu maradhi mbali mbali “. Alisisitiza Dr. Shein.

Rais wa Zanzibar aliwasisitiza wahitimu wa Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya Zanzibar kuchangamkia ajira zinazotolewa na Serikali na Sekta Binafsi wakitambua kwamba Hospitali zote zina lengo la kuimarisha huduma za afya kwa faida ya Wananchi.

Kuhusu upatikanaji wa ruzuku zinazotolewa na Serikali kwa taasisi za umma Rais Shein alisema changamoto kubwa ya mahitaji ya Serikali zinasababisha ruzuku hizo kutofikia kiwango halisi kinachoweza kuridhisha taasisi hizo.

Hata hivyo Rais wa Zanzibar aliiagiza Wizara ya afya pamoja na Wizara ya Fedha Zanzibar kufanya mapitio ya ruzuku inayopewa Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya Zanzibar.

Alieleza kwamba endapo ikithibitika kuwa kiwango kinachotolewa ni kidogo, uwe9o mjadala na kuangaliwa utaratibu wa namna ya kuweza kuwaongezea ili chuo hichi muhimu kiweze kuendesha mipango ya maendeleo kinachijipangia.

Aliupongeza Uongozi wa Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya Zanzibar kwa kutoa mchango mkubwa katika utekelezaji wa mipango ya Serikali tokea kilipoanzishwa katika kuimarisha sekta ya afya kwa misingi iliyowekwa na waasisi wa Afro Shirazy Party wakati wa kupigania uhuru wa Nchi hii.

Alisema chuo hicho hivi sasa kimekuwa chem chem ya kutoa wataalamu mbali mbali wanaohitajika katika Hospitali na Vituo tofauti vya Afya hapa Nchini kwa lengo la kuwapatia Wananchi huduma bora za Afya.

Alieleza kwamba Taifa kwa sasa limepiga hatua kubwa kwa kusomesha wataalamu wazalendo wenyewe jambo ambalo limesaidia kuokoa fedha nyingi ambazo zingelazimu kulipa kwa ajili ya kuwasomesha wataalamu hao nje ya Nchi kama ilivyokuwa ikifanywa hapo zamani.

Mmoja wa wahitimu hao Faika Karim Zam kwa niaba ya wenzake wameuomba Uongozi wa Chuo hicho kuanzisha mafunzo ya ngazi ya Shahada { Diploma } kwa nia ya kuwapunguzia gharama za kutafuta elimu hiyo nje ya nchi.

Faika Karim alisema uanzishwaji wa mafunzo hayo ni vyema ukaenda sambamba na upatikanaji wa vifaa vya kufundishia, huduma za Maktaba,kukabiliana na upungufu wa Walimu wa kudumu na watakuwa tayari kuusaidia Uongozi huo ili wanafunzi wanaofuatia wafaidike na Mpango huo.

Alifahamisha kwamba hatua hiyo itawawezesha wanafunzi wanaoingia kwenye Chuo hicho muhimu kupata taaluma ya kisasa inayokwenda sambamba na mabadiliko ya dunia yaliyopo hivi sasa ya sayansi na Teknolojia.

Mapema Mkuu wa Chuo cha Taalum za Sayansi za Afya Zanzibar Dr. Haji Mwita Haji alisema Uongozi wa Chuo hicho kupitia Baraza lake umeamua kuongeza majengo zaidi ili kuwahudumia vyema wanafunzi wanaoamua kujiunga na chuo hicho sambamba na mahitaji ya ongezeko la Hospitali na vituo vya Afya Nchini.

Dr. Mwita alisema hatua hiyo inalenga kukijengea hadhi na sifa chuo hicho kilichoanzishwa mwaka 1938 kikiwa miongoni mwa vyuo vichache barani Afrika vilivyokuwa vikitoa elimu ya Afya licha ya kwamba hakikuwa na makaazi ya Kudumu.

Aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Oman kwa muono wao wa kuenga majengo ya kudumu ya chuo hicho ambayo yanatoa fursa kwa Chuo hicho katika muelekeo wake wa matayarisho ya kuwa kitengo cha Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar { SUZA }.

Akimkaribisha Mgeni rasmi katika ufungaji wa Mahafali hayo ya 22 ya Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya Zanzibar, Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mh. Mahmoud Thabit Kombo aliwaomba wauguzi kufuata maadili ya kazi zao ili kupunguza au kuondosha kabisa malalamiko yanayotolewa na wananchi.

Mh. Mahmoud alisema lugha zao kwa wagonjwa ndio kitendo kilichompa wakati mgumu alipokuwa akijibu maswala ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika Vikao vya Baraza hilo vilivyokuwa vikiendelea kwa muda wote wa miaka mitano iliyopita.

Naibu Waziri wa Afya pia aliwapongeza Wafanyakazi wa Sekta ya Afya wa muda mrefu walioamua kujisajili na kupata taaluma na hatimae kufanikiwa kuwa miongoni mwa wahitimu wa mkupuo wa 22 wa Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya Zanzibar.

Alisema Watendaji wote kwa sasa wanapaswa kubadilika kwenda na wakati unaokwenda sambamba na teknolojia ya kisasa ya sayansi iliyopo ulimwenguni ambayo humuwezesha mfanyakazi kufanya kazi mahali popote Duniani.

Wahitimu 440 wamefanikiwa kupata stashahada katika fani saba za sekta ya afya ambazo ni pamoja na Afisa Tabibu wa Afya ya Kinywa na Meno, Afisa Tabibu, Afya ya Mazingira, Uuguzi na Ukunga, Utabibu wa Maabara,Madawa pamoja na Ufundi Sanifu wa Vifaa vya Hospitali.

Katika Mahafali hayo ya 22 ya Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya Mgeni rasmi pia alifanikiwa kutoa vyeti Maalum kwa Wanafunzi bora zaidi wa kila fani katika mafunzo hayo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top